Kamati TFF yamng'oa Bwire bila kuhojiwa

Muktasari:

Wagombea katika uchaguzi wa Bodi ya Ligi, wanatarajiwa kufanyiwa usaili leo na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Desemba Mosi.

Dar es Salaam. Uchaguzi wa Bodi ya Ligi unatarajiwa kufanyika Desemba Mosi na tayari mgombea nafasi ya mwenyekiti James Bwire ameenguliwa kwenye kinyang'anyiro hicho kabla hata ya kufanyiwa usaili na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Uchaguzi huo unafanywa kwa usiri mkubwa ulikuwa na wagombea watatu ambao ni Steven Mguto (Mwenyekiti wa Coastal Union), Emmannuel Kimbe (Mkurugenzi Mtendaji wa Mbeya City) na Bwire (Mkurugenzi wa Alliance FC).

Usaili wa wagombea hao unafanyika leo Ijumaa hivyo ni wagombea wawili pekee Mguto na Kimbe ndiyo watafanyiwa usaili huo jijini Dar es Salaam baada ya Bwire kuondolewa.

"Hata Kimbe wanaweza kumpiga chini wanataka abaki Mguto pekee ili asiwe na mpinzani maana lengo ni kumpa hiyo nafasi," kilisema chanzo hicho kutoka kwenye Kamati ya Uchaguzi.

Upande wa Bwire alikiri kuondolewa kwenye kinyang'anyiro hicho kwamba alitumia barua pepe ya kumweleza kuwa hana sifa kikanuni kugombea nafasi hiyo.

"Kiukweli sikuandikiwa ni kanuni ipi, kilichoandikwa tena kwa ufupi tu ni kwamba sina sifa za kikanuni kugombea nafasi hiyo, ilinibidi nikae kimya tu kwani niliona italeta mgogoro usiokuwa na maana, kwani wao ndiyo wanaelewa sababu zaidi," alisema Bwire.