Kama vipi! tukutane Anfield

LIVERPOOL ENGLAND. USITUTISHE. Utamu wa Ligi Kuu ya England utaendelea leo kwenye mchezo mkali kati ya Liverpool ambayo itakuwa nyumbani dhidi ya Arsenal katika mechi inayotarajiwa kupigwa saa 4:00 usiku.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa wa kisasi kwa Liverpool ambayo imepoteza michezo miwili mfululizo iliyopita ikiwa pamoja na ule wa mwisho wa Ngao ya Jamii ambapo ilifungwa kwa mikwaju ya penalti, baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Tangu Oktoba, 1983 timu hizi zimekutana katika mechi 230, Arsenal imeshinda 80, sare 61 na imefungwa 89, huku Liverpool ikishinda 89, sare 61 na kupoteza 80.

Lakini katika michezo 11 ya mwisho Liverpool inatamba kwa kushinda mechi sita huku tatu ikitoka sare na mbili pekee ndio Arsenal ilishinda.

Jambo linalozidisha joto kwa Arsenal ni kwamba haijawahi kupata ushindi katika dimba la Anfield tokea Septemba, 2012 ambapo ilishinda mabao 2-0, baada ya hapo imepoteza mechi sita na kutoka sare mara mbili.

Kuelekea mchezo huo, kocha wa kikosi cha Arsenal alifunguka kwa kusema wataingia kwenye uwanjani na kucheza vile ambavyo wanacheza na ana matumaini ya kushinda. “Tunachotakiwa kukifanya ni kuonyesha ubora na muendelezo wa matokeo mazuri, lakini sisi tutapambana pale ambapo tunaweza na kitu pekee tutakachofanya ni kuhakikisha tunashinda na tutajitahidi kufanya vizuri kuliko msimu uliopita,” alisema Arteta.

“Wana kikosi cha wachezaji ambao hawaridhiki wala kukata tamaa, hata wakiwa wanaongoza au wameongozwa kwa mabao 2-0, 3-0 na 4-0, na kutokana na hili unapaswa kumpongeza kocha na benchi la ufundi,” aliongeza.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp naye alisema, Arteta ni miongoni mwa makocha ambao wamedhihirisha ubora wao kwa kipindi kifupi ambacho ameichukua Arsenal na kumewapo na mabadiliko makubwa.

“Wanacheza mfumo wa 5-4-1 ambao unawafanya wachezaji wote kuwa sehemu ya ulinzi wakati timu inashambuliwa, hiyo inakuwa ngumu kwao kuacha mianya na hata timu pinzani inapofanya mashambulizi ya kushtukiza,” alisema Klopp.

“Nafikiri nitatumia muda mrefu kuzungumzia ubora walionao kwa kuwa wanastahili, lakini ninaamini tuna nafasi kubwa ya kushinda katika mchezo huo, kwani licha ya ubora wao sisi pia tuna timu nzuri,” aliongeza.

Timu hizi zimeshinda mechi zote mbili za kwanza za Ligi Kuu ya England msimu huu na Arsenal imefunga mabao matano na kufungwa bao moja wakati Liverpool imefunga mabao sita na kuruhusu nyavu zake kutingishwa mara matatu katika mechi zao tatu za kwanza za msimu huu kufikia sasa. Hivyo Arsenal iko juu ya Liverpool kwa tofauti ya mabao ya kufunga na ya kufungwa.

Baada ya mchezo huo wa leo, Arsenal italazimika kurudi tena Anfield kwa ajili ya mchezo wa Carabao Cup, Oktoba 1, Saa 3:45 usiku. Baada ya hapo itacheza dhidi ya Sheffield United katika Ligi Kuu, kabla ya kuivaa Manchester City Oktoba, 17. Liverpool nayo baada ya mchezo huo na ule wa Carabao itaendelea na Ligi Kuu ambapo itacheza dhidi ya Aston Villa Oktoba 4, na Everton, Oktoba 17 ambazo zote itachezea ugenini.

Mchezo mwingine ambao utapigwa leo ni Fulham inayoshika nafasi ya 20, baada ya kupoteza mechi mbili za mwanzo dhidi ya Aston Villa iliyopo nafasi ya tisa baada ya kushinda mchezo wake wa kwanza.

Safu za kutisha za ushambuliaji zitapimwa leo.