Kakolanya ataka rekodi yake

Muktasari:

  • Mpaka hivi sasa Kakolanya ameruhusu nyavu yake iguswe mara moja tu katika michezo 5 aliyocheza ya Ligi Kuu.

KIPA Beno Kakolanya wa Yanga anataka kutengeneza rekodi yake ya kipekee kwa kutoruhusu magoli mengi akiwa na kikosi hicho msimu huu.

Kakolanya akiwa ameidakia timu hiyo michezo mitano ya Ligi Kuu mpaka hivi sasa, ameruhusu bao moja tu kutingisha nyavu zake dhidi ya Mtibwa Sugar uliomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 2-1. Akizungumza na Mwanaspoti, Kakolanya alisema kuwa hali hiyo inamfanya azidi kujituma zaidi uwanjani ili kuhakikisha anaendeleza rekodi yake na kujiweka kwenye mazingira ya kukuza kipaji chake.

“Hili ni jambo ambalo kipa yoyote anapenda kuwa nalo, najisikia furaha lakini pia sio kwangu tu bali timu nzima kwa sababu inafanya vizuri,” alisema.

Aliongeza zaidi kwamba siri ya yeye kufanya vizuri ni kuwapanga vizuri na mabeki wake uwanjani na kuhakikisha kwamba, hata ikitokea kosa kwa mmoja basi mwingine analiziba. “Huwa nazungumza sana ninapokuwa uwanjani kuhakikisha kila mmoja anafanya kazi yake vizuri, nashukuru wapo makini na tunakwenda sawa,” alisema.