Kakolanya arejeshwa kikosini, Simba wakiivaa Namungo

Wednesday July 8 2020

 

By THOMAS NG'ITU

KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck amemrejesha kipa Beno Kakolanya katika kikosi cha kwanza kitakachocheza dhidi ya Namungo leo Jumatano kuanzia saa 10:00 jioni, mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara inachezwa Uwanja wa Majaliwa, Wilaya ya Ruangwa.

Awali ilielezwa kwamba kipa huyo yupo katika mgogoro na kocha wa makipa Mohamed Muharami, baada ya kusemekana kwamba kocha huyo ameeleza Kakolanya kushuka kiwango na kuongezeka uzito na hivyo nafasi yake ilichukuliwa na Ally Salim huku kipa namba moja akiendelea kuwa Aishi Manula.

Kakolanya aliondolewa kabisa kwenye benchi na kukosa mechi dhidi ya Ruvu Shooting, Mwadui, Mbeya City, Prisons, Azam (FA) na Ndanda.

Katika kikosi hicho kinachocheza na Namungo mchezo ambao utatumika pia Simba kukabidhiwa kombe lao la ubingwa wa ligi, Sven amefanya mabadiliko mengi baada ya nafasi ya beki wa kati kuwachezesha Yusuph Mlipili na Tairone Santos ambao awali walikuwa hawapati nafasi ya kucheza namba hizo kuchezwa na Kennedy Juma na Pascal Wawa.

Safu ya kiungo amemuanzisha Mzamiru Yassin, Francis Kahata, Said Ndemla na Miraj Athuman huku safu ya ushambuliaji akipangwa Meddie Kagere badala ya John Bocco.

Eneo la kiungo ameweka sura mpya na kuwaondoa Gerson Fraga, Luis Miquissone, Jonas Mkude na Bocco waliocheza mechi iliyopita dhid ya Ndanda.

Advertisement

Upande wa wachezaji wa akiba ni Ally Salim, Gadiel Michael, Sharaf Shiboub, Deo Kanda, Hassan Dilunga, Cyprian Kipenye na Shiza Kichuya.

 

Mabadiliko haya ni nafasi kwa wachezaji wengine ambao hawakupata nafasi ya kucheza mechi zilizopita za Ligi na Kombe la Shirikisho.

Advertisement