Kaka wa Samatta akerwa na maswali

WATU buana, wana maudhi sana! Kiungo mshambuliaji wa KMC, Mohamed Samatta amesema hakuna changamoto kubwa anayokutana nayo na wakati mwingine kumuudhi kama kuulizwa na watu ni kweli umezaliwa na Mbwana Samatta 'Samagol'.
Mohamed, aliye kaka wa nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga Aston Villa ya England, amesema kero hiyo amekuwa akikutana nayo mara kwa mara ya kuulizwa swali hilo hilo.
Amesema swali hilo amekumbana nalo kutoka kwa mashabiki, wachezaji wenzake na watu wa mitaani na kumnyima raha kwani hakuna jambo la ajabu yeye kuzaliwa tumbo moja na Samagol.
"Kuna sehemu nyingine inakuwa inahitajika kuonyesha kitambulisho, mtu anakuuliza wewe ni ndugu yake na Samatta nikisema mdogo wangu hawaamini, inaudhi kwani siwezi kung'ang'ania mtu asiye ndugu yangu," amesema.
Kiungo mshambuaji huyo aliyewahi kukipiga Mgambo JKT, Tanzania Prisons na Mbeya City amesema jambo ambalo watu wanapaswa kutambua ni kwamba Mungu anaamua kutoa ridhiki kwa kila mtu ila zinatofautiana akimaanisha mafanikio ya ndugu yake hayawezi kuwatenga.
"Mungu kampa fungu tofauti na mimi ila haitabadilika kuwa kaka yake, ninachopenda ni unyenyekevu wake, kwangu ila kuna watu wanashindwa kuamini kama mimi na Mbwana ni ndugu, inaniudhi sana," amesema.
Mohamed amewahi kucheza sambamba na Mbwana Samatta walipokuwa African Lyon, kabla ya mdogo wake kunyakuliwa na Simba kisha kwenda TP Mazembe aliyodumu nao kwa misimu mitano na baada ya kutimkia Genk ya Ubelgiji na sasa anakpigika Villa inayoshiriki Ligi Kuu (EPL).
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka ya 31 kwa sasa ameifungia KMC mabao mawili kwenye ligi hiyo iliyosimamishwa ili kupisha janga la ugonjwa wa covid-19 unaoenezwa na virusi vya corona.