Kagere kaanza balaa mapemaa

Muktasari:

Wakati Kagere akiuwasha moto huo wa kufunga mabao, winga Kahata aliyesajiliwa na kikosi hiko akitokea Gor Mahia hakuwa nyuma katika kuonyesha ufundi wake wa kutengeneza nafasi za mabao huku wakati mwingine akifunga mwenyewe.

KIKOSI cha Simba kinaendelea kujifua hapa kambini Rustenburg kabla ya kurejea Bongo kuonyesha makali kwenye Tamasha la Simba Day.

Lakini, wakati nyota wakiendelea kujifua waliwaacha nyuma mastaa wanne, akiwemo Meddie Kagere ambaye ndani ya siku mbili tu za mazoezi licha ya kuchelewa kujiunga na wenzake tayari ameanza mambo ya hatari.

Kagere, ambaye ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita akimaliza na mabao 23, hakutaka kupata muda wa kutosha katika mazoezi ya siku mbili alionesha makali yake mapema.

Katika mazoezi hayo ya kucheza timu mbili tofauti Kocha wa Simba Patrick Aussems akiwa na msaidizi wake Denis Kitambi alitaka kuwaona viungo wa kati na pembeni wakipiga pasi za mwisho kwa washambuliaji na hapo ndio Mrwanda huyo akaonyesha shughuli kwa mabeki msimu ujao itakuwa moto.

Katika zoezi hilo Aussems alimuweka Kagere kama mshambuliaji wa mwisho, ambaye alikuwa akipachika mipira nyavuni kwenye kila nafasi anayopata. Alikuwa akifunga mabao kutumia kichwa na miguu yote kama ilivyo kawaida yake alivyokuwa akifanya kwenye Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika na mashindano mengine ambayo Simba ilioshiriki msimu uliopita.

Wakati Kagere akiuwasha moto huo wa kufunga mabao, winga Kahata aliyesajiliwa na kikosi hiko akitokea Gor Mahia hakuwa nyuma katika kuonyesha ufundi wake wa kutengeneza nafasi za mabao huku wakati mwingine akifunga mwenyewe.

Mwanaspoti ambalo limepiga kambi hapa Rustenburg linafahamu Kahata ambaye ni miongoni mwa usajili uliokuwa mapendekezo ya Aussems alikuwa na maelewano na washambuliaji Kagere, John Bocco na Wilker Henrique ambao walikuwa wakitumia vyema krosi na pasi ambazo alizokuwa akiwapatia.

Kwa upande wake, Aussems alisema usajili uliofanywa na kikosi hicho ni mzuri kulingana na mapungufu yalikuwa katika timu msimu uliopita na kuwepo kwa wachezaji wengi wenye uwezo kutaongeza ushindani wa kuwania nafasi ya kucheza kwenye timu.

“Mazoezi haya ambayo tunaendelea kufanya yatatoa mwanga ya kile ambacho tunakwenda kukifanya katika mechi za kimashindano ndio maana kila mchezaji anafanya kila anachoweza ili kuonesha kile ambacho anacho jambo ambalo ni zuri kwetu benchi la ufundi,” alisema Aussems.

MSIKIE KAGERE

Kagere alisema nafasi yake ni mshambuliaji na jukumu lake la kwanza ni kufunga mabao kila ambapo atakuwa anapata nafasi.

“Kama mshambuliaji natakiwa kufunga kila nafasi ambayo nitaipata kutokana nafasi yangu ambayo nacheza hilo ndio jukumu langu la kwanza lakini hata kama nikishindwa niweze kuwatengenezea nafasi wenzangu wafunge,” alisema.

“Kuhusu kuwa mfungaji bora tena msimu ujao hilo si la kwanza kwangu kwani nataka kuona timu inafikia malengo yake ambayo imejipangia kwani ikiweza kufanya hivyo ndio malengo ya kila mchezaji yataweza kutimia,” alisema Kagere.

KAHATA NAYE

Kahata hakuwa nyuma alieleza amekuja Simba ambayo ina wachezaji wazuri wenye uwezo hivyo lazima nifanye kinachotakiwa ili kushindania nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza.

“Nimekuja Simba wakati sahihi, nimekionesha kile ambacho ninacho katika mazoezi na hata kwenye mechi nikipata nafasi nitakuwa nafanya, hivyo ili niweze kucheza mara kwa mara,” alisema Kahata, ambaye aliongezea anafahamu mashabiki wa timu hiyo wanatamani kuona hilo kutoka kwake.