Kagere aamsha shangwe Iringa

Muktasari:

Straika wa Simba, Mnyarwanda Meddie Kagere amewaambia mashabiki wa kikosi chake wa Iringa wakae mkao wa kula kwa sababu wanakwenda kushinda mechi yao ya Jumamosi dhidi ya Lipuli FC.

KINARA wa mabao wa Simba na Ligi Kuu Bara, Mnyarwanda Meddie Kagere ameamsha shangwe la maana kwa mashabiki wa kikosi chake walio Iringa kuwa wamekwenda kuwapa raha.
Kagere anayeongoza msimamo wa wafungaji bora wa ligi na mabao 12, amesema hayo akiwa katika maandalizi ya kuwavaa Lipuli FC.
Simba itacheza na Lipuli FC Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Samora Iringa.
"Watu wangu wa Iringa tupo njiani (maneno ya Kagere jana Alhamisi) hivyo jiandaeni kwa furaha, ni mwendo wa raha tu,"alisema Kagere.
Simba imesafiri kwenda Iringa jana Alhamisi ikitokea Morogoro ambako ilikuwa na mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar waliyoichapa mabao 3-0, juzi Jumanne kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Kama Simba yenye pointi 53, baada ya kucheza mechi 21, itashinda mchezo huo, wataendelea kutamba kileleni mwa Ligi Kuu, Azam FC itaendelea kushika nafasi ya pili na pointi 44, wakati Yanga iliyocheza mechi 19, ipo nafasi ya tatu na pointi 38.
Singida United ndio inashika mkia na pointi 11, Mbeya City ya pili kutoka mkiani, imefungana pointi na  Mwadui FC iliyo ya tatu kutoka mkiani ambazo ni 18.