Kagere: Subirini tuwape raha Shirikisho

Friday July 24 2020

 

By Meddie Kagere

AGOSTI 2, katika mkoa wa Rukwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela utapigwa mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC), kati ya Simba waliotinga kwenye hatua hiyo baada ya kuwafunga watani wao Yanga mabao 4-1, katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Namungo ambao waliwafunga Sahare All Stars bao 1-0.

Katika kolamu yangu wiki hii napenda kuzungumzia mechi hiyo ambayo ndio itakuwa hitimisho la msimu huu kwani nafahamu kila timu itakuja na malengo ya kutaka kuondoka na ushindi ili kutwaa ubingwa na kubeba taji.

Mechi yenyewe itakuwa tofauti kwanza upande wetu tumefanikiwa malengo ya msimu huu kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, tumetwa Ngao ya Hisani lakini tumeabakisha lengo moja la kutwaa ubingwa wa kombe hili la ASFC.

Hivyo hivyo kwa wapinzani Namungo nao wataingia na malengo ya kutaka kutufunga ili kutwaa taji kwani timu hiyo ni msimu wake wa kwanza kucheza ligi lakini maandalizi na kikosi chao bora ndio yamewafikisha katika hatua hii na hata ukiwaangalia katika msimamo wapo kwenye nafasi za juu.

Kwetu Simba tutaingia kana kwamba hatuna wasi wasi huku tukicheza kwa ustadi na ustaarabu mkubwa tukifanya mashambulizi mengi ili kutaka kumaliza mchezo mapema. Jambo hilo linachangiwa na matokeo ambayo tumeyapata mpaka kufikia hapa.

Kwanza kabla ya kucheza na Namungo katika mechi ya nusu fainali tulimfunga mtani wetu Yanga, ambaye tulikuwa tunatamani litokee hilo siku nyingi nyuma kutokana tulikutana nao mara mbili katika ligi msimu huu na tumeshindwa kupata pointi tatu dhidi yao.

Advertisement

Ukiangalia matokeo yetu ambayo tunayo katika ligi ni mazuri mpaka kufikia hatua ya kutwaa ubingwa lakini kuna rekodi mbalimbali ambazo tumefanikiwa kuziweka mpaka kukamilisha msimu huu.

Kwa maana hiyo tutakuwa na utulivu na umakini mkubwa tofauti na katika mechi nyingine nyingi ambazo tumecheza huko nyuma pia tunaweza tukawa tunabadilika ndani ya uwanja kulingana na wapinzani wetu Namungo ambavyo watakuwa wanacheza.

Kutokuwa na presha kwetu wala wasiwasi wa aina yoyote itamfanya kila mchezaji ambaye atapata nafasi ya kuiwakilisha timu acheze kwa kujiamini na kufanya kila ambalo anaweza ili kuona timu inafanikiwa kupata ushindi na kutwaa kombe hilo.

Eneo la kuchezea kwenye uwanja ambao tutautumia sijaufahamu kwa maana hatujawahi kufika huko lakini kama litakuwa linaruhusu kucheza mpira wetu wa kupasiana pasi za chini na kumiliki mpira kama vile ambavyo tunacheza kwenye Uwanja wa Taifa au Uhuru litakuwa jambo jema zaidi kwetu lakini kama ikiwa tofauti na hivyo ni wazi linaweza kuwa jambo gumu kwetu.

Kama wanajeshi tupo tayari kupambana katika mazingira yoyote yale iwe mvua iwe jua ili kuona mafanikio ya Simba kuchukua ubingwa huo wa ASFC, unawezekana kama ambavyo tuliweka malengo mwanzo wa msimu.

Kwa upande wa wapinzani Namungo wao kwanza tayari wataingia katika mechi hiyo wakiwa na uhakika wa kucheza mashindano ya kimataifa msimu ujao ila ambacho watataka ni heshima ya kwenda kucheza michuano hiyo wakiwa mabingwa wa ASFC.

Namungo watakuja kwa nguvu, kushambulia kwa haraka, watakuwa na matumizi ya nguvu kutaka kushindana na wachezaji wa Simba ili kuweza kutuzidi kama walivyofanya katika mechi ya ligi ambayo tulicheza nyumbani kwao. Hilo tunalitambua na tutalifanyia kazi.

Ushindani ambao utatokea kwa sababu timu zote zitakuwa zimejipanga huku kila mmoja akiwa na uhakika wa kucheza mashindano ya kimataifa msimu ujao. Mashabiki watapata raha na burudani ya kutosha kutokana na umahiri ambao timu zote wachezaji wake watakuwa wakionyesha.

Naona utakuwa mchezo mgumu kwa timu zote kutokana na rekodi hizo ambazo nimeeleza na ushindani wa aina yake lakini kama Simba tumejipanga kuonyesha burudani ambayo itaambatana na ushindi ndani yake ili mashabiki wetu kumaliza kwa furaha msimu huu.

Kama wachezaji wa Simba tunaendelea na majukumu yetu kwa sasa kama ambavyo tutafanya katika mechi hiyo kila mmoja kupambana kadri ambavyo anaweza kulingana na mahitaji ya nafasi yake ili kuona tunawazidi Namungo na kupata ushindi.

Kwa maana hiyo tunaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kulingana na nafasi ambazo zitapatikana kwao wakati huo huo wakizingatia maagizio ya wataalamu kujikinga na janga la virusi vya corona ili mbali ya kupata burudani kila mmoja awe salama kwa kujilinda mwenyewe na pia kumlinda mwenzake.

Advertisement