Kagere, Okwi, Bocco kuikosa Simba

Muktasari:

Kikosi cha Simba kabla ya kucheza na Mazembe katika mechi ya kwanza watakuwa na mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao utapigwa Aprili 3, katika uwanja wa Jamuhuri Morogoro ambao watautumia kama uwanja wa nyumbani.

KIKOSI cha Simba kitarejea mazoezini kesho Jumatatu katika uwanja wa Boko Veterans kwa ajili ya kujiwinda na mechi ya robo fainali dhidi ya TP Mazembe ambayo itachezwa hap nchini Aprili 6.
Kikosi hiko cha Simba ambacho kilipewa mapumziko ya siku tano na kocha Patrick Aussems kitaanza mazoezi asubuhi ya kesho Jumatatu lakini kitawakosa mastraika wake watatu Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na John Bocco.
Mastraika hao watakosekana kutokana na kuwa katika majukumu ya timu zao za Taifa na wamepewa mapumziko ya siku moja kabla ya kuanzia Jumanne kila mmoja anatakiwa kuripoti kambini.
Kikosi cha Simba kabla ya kucheza na Mazembe katika mechi ya kwanza watakuwa na mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao utapigwa Aprili 3, katika uwanja wa Jamuhuri Morogoro ambao watautumia kama uwanja wa nyumbani.
Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema mara baada ya kuanza mazoezi hawatakuwa na muda wa kupoteza kwani watakuwa na muda mfupi ambao wanatakiwa kucheza mechi nyingi.
"Hatuna muda wa kupoteza tena ratiba ya ligi tunatakiwa kucheza mechi kila baada ya siku tatu ambayo tutashindwa kuwa na muda wa kufanya mazoezi zaidi ya kufanya tu yale ya kuweka miili sawa," alisema Aussems.