Kagere, Mayanga watwaa tuzo za VPL

Muktasari:

Shirikisho la Soka Tanzania kupitia mtandao wa Twitter wamewatangaza mshambuliaji na kocha bora wa mwezi Agosti Ligi Kuu Bara.

Dar es Salaam. Mshambuliaji  wa kimataifa wa Simba, Meddie Kagere ambaye  ameunza msimu huu  kwa kishindo ndiye aliyefungua tuzo za uchezaji bora wa mwezi  Ligi Kuu Bara.
Kagere alianza ligi ya VPL kwa kuifungia timu yake ya Simba mabao mawili dhidi ya JKT Tanzania, ikiibuka na ushindi wa mabao 3-1, kitu kilichompa ushindi dhidi ya washambuliaji wawili kwenye kinyang'anyiro hicho.
Katika kinyang'anyiro hicho Kagere alikuwa anashindana na Lucas Kikoti kutoka Namungo na Seif Karie wa Lipuli FC.
Kupitia mtandao wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wamemtangaza Kagere kutwaa tuzo ya VPL kwa msimu huu ambao Vodacom wamerejea kuwa wadhamini.
Ukiachana na Kagere kuchukua tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Agosti, kocha bora amekuwa Salum Mayanga wa Ruvu Shooting ambaye aliisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga kwenye mechi yao ya kufungua pazia la msimu mpya.
Kocha Mayanga alikuwa anashindana na Mecky Maxime (Kagera Sugar) na Hitimana Thiery wa Namungo ambao walishinda mechi zao za fungua pazi la ligi ya VPL.