Kagera wawapania Yanga

Wednesday September 16 2020

 

By SADDAM SADICK

HADI sasa Kagera Sugar imeshacheza mechi mbili huku ikiwa haijaonja ushindi wowote katika Ligi Kuu msimu huu, sasa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mecky Maxime ameibuka na kusema wanaanza na Yanga kutembeza dozi.

Kagera Sugar ilianza kwa kipigo cha bao 1-0 nyumbani dhidi ya JKT Tanzania kisha kuambulia suluhu mbele ya Gwambina na sasa wanajiandaa kuwakaribisha Yanga, mchezo utakaopigwa Jumamosi katika dimba la Kaitaba mjini Bukoba.

Maxime ambaye alichomoa kujiunga na Yanga kama Kocha Msaidizi dakika za mwisho, alisema bado hawajapata kile wanachokihitaji, hivyo huenda kazi ikaanzia katika mchezo wao dhidi ya Yanga kutembeza mkong’oto na kurejesha furaha.

“Hii ni Ligi tulianza na matokeo hayo, lakini tulihitaji ushindi kila mechi, hivyo tunatarajia kuanza kazi na Yanga ili kuleta nguvu na morali kikosini hata kwa mashabiki,” alisema.

Alisema pamoja na matokeo waliyopata kutoridhisha, lakini si kwamba vijana wake walizidiwa chochote kiufundi, isipokuwa ishu ya miundombinu ya uwanja na bahati kutokuwa kwao ndio iliwapa matokeo hayo.

“Mechi kama ya Gwambina kila mmoja aliona ishu ya uwanja ulivyokuwa, mpira haukutulia, lakini hata ile tuliyiopoteza kwa JKT, haikuwa bahati yetu kwa sababu muda wote tulimiliki mpira sisi” alisema.

Advertisement

Advertisement