Kagera Sugar yaishusha Simba kileleni

Saturday September 21 2019

 

By WAANDISHI WETU, MWANZA

KAGERA Sugar imeshusha Simba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kushinda mechi yake ya leo Jumamosi dhidi ya Mbao FC.
Mechi hiyo iliyochezwa uwanja wa Nyamagana imemalizika kwa ushindi wa bao 1-0 ikiwa ni mechi ya tatu ya Ligi Kuu upande wa Kagera Sugar ambapo mechi zote wameanzia ugenini.
Kagera Sugar imekusanya pointi tisa wakati Simba iliyokuwa inaongoza kwa pointi sita ikiwa imecheza mechi mbili imeshuka hadi nafasi ya tatu huku Namungo yenyewe ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi saba.
Namungo wamecheza mechi tatu, wameshinda michezo miwili ambapo leo wamelazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Mwadui FC ambao wanashika nafasi ya tano wakiwa na pointi tani huku wakicheza mechi tatu, wameshinda mechi moja na sare mbili.
Kagera Sugar walipata bao hilo dakika ya 38 baada ya mabeki kujifunga wakati wakizuia mpira wa faulo ulionyooshwa na kiungo, Awesu Awesu.
Awesu alipewa jukumu hilo lililotokana na David Luhende kuangushwa nje kidogo ya eneo la 18 huku Mbao wakijaribu kulazimisha mashambulizi lakini ngome ya Kagera Sugar ilikuwa imara kuchomoa hatari zote hadi dakika 90.
Kwa matokeo hayo Kagera Sugar  wameweka rekodi safi ya kushinda mechi mfululizo ugenini ambapo awali waliifunga Biashara United bao 2-0, waliipiga Alliance FC bao 2-1.

Imeandikwa na Saddam Sadick, James Mlaga na Masoud Masasi.

Advertisement