Kabwili apata dili huko Sudan

Muktasari:

  • Kabwili alithibitisha kutaka kwenda Sudan, lakini akisema hata viongozi wake wa sasa walikuwa wakizungumza naye ili abaki Jangwani na bado hajaamua afanye nini.


YANGA huenda ikapata pengo jingine katika kikosi chake baada ya kipa wao Ramadhani Kabwili kupata dili la kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Sudan.

Ofa ya Kabwili imekuja wakati baadhi ya nyota wake wakianza kutimka kikosini akiwamo Heritier Makambo, Ibrahim Ajibu na Maka Edward waliopata shavu katika klabu za Horoya AC ya Guinea, Simba na Spartaks Jermala ya Latvia.

Mwanaspoti unafahamu wakati ofa hiyo ikiwa mezani kwa chipukizi huyo aliyesajili kutoka Senegeti Boys iliyoshiriki Afcon U17 2017, tayari Kabwili alikuwa akipigiwa hesabu na Namungo iliyopanda Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.

Kabwili alithibitisha kutaka kwenda Sudan, lakini akisema hata viongozi wake wa sasa walikuwa wakizungumza naye ili abaki Jangwani na bado hajaamua afanye nini.

“Inawezekana kwenda huko Sudan au timu nyingine na hata kubaki hapa Yanga yote ni ya kweli ila ikifika Juni 24, naweza kuwa na majibu sahihi ya wapi nitakuwa msimu ujao.”

Kabwili aliongeza angependa kupata changamoto mahali pengine ikishindana kubaki Jangwani.