Kabla ya kikosi Yanga inahitaji ‘usajili’ wa viongozi

Thursday July 23 2020

 

By KHATIMU NAHEKA

Taifa sasa limegeukia siasa kidogo katika kuwania nafasi mbalimbali kupitia vyama vya siasa, huko kuna matokeo ya kustajaabisha kama vile katika soka. Unaweza kuona mbuyu unaangushwa kwa kura ambazo hata kama wapiga kura wangekuwa watu wa familia yake unaweza usiamini namba wanazoambulia.

Kuwania huko wapo pia watu wa michezo mbalimbali ambao kura zimetosha na wengine hazikutosha, ingawa mambo tunaambiwa na wajuzi wa siasa kwamba mchakato bado unaendelea. Acha niwapongeze walioibuka kidedea lakini niwape pole pia walioanguka, wajifunze kupiga hesabu vizuri.

Kuwania huko nafasi na haya yanayoendelea wapo pia Yanga wamejificha na aibu ya msimu kwa kutoka bila taji lolote. Kwa mashabiki wameamua kujificha humo kupoza machungu angalau kujiliwaza, lakini kwa viongozi nao wameamua kutafuta kichaka cha kupunguza makali ya kuchukiwa.

Yanga imeanguka vibaya na rekodi zinaonyesha huu ni msimu wa tatu wanatoka bila taji, sio afya sana kwa klabu yao, lakini kuna la kujifunza kupitia mafanikio haya kuhamia upande wa pili kwa watani wao, Simba, ambao wametawala misimu hii mitatu wakati sasa wakilitafuta taji la tatu kwa msimu mmoja wakienda kucheza Fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Namungo FC.

Sitawaacha nitaendelea kuwakumbusha mashabiki na wanachama wa Yanga kwamba, anguko lao kubwa limetokana na uamuzi wao wa kuwachagua baadhi ya viongozi ambao hawakuwa na hadhi ya kuiongoza klabu yao.

Yanga hakuna kinachoeleweka katika uongozi wao, hatua kubwa katika maisha yao imekuwa ni migogoro na kutimuana. Timu imesambaratika kiutendaji na utulivu wa kiutendaji umekuwa mdogo.

Advertisement

Hali iliyomo Yanga hakika inathibitisha kwamba kuna kundi kubwa la viongozi hawakuwa watu sahihi kuchukua hatamu hizo, wanaoonekana kuwa na tija ni wachache ambao nao wanafunikwa na wengi wasiojiweza.

Hili linajulikana, leo niishie hapo, lakini muhimu ambalo wanapaswa kulifanya sasa ni kuangalia wapi wameangukia na kipi kifanyike.

Naona wengi wanadhani akili kwa Yanga ni kufanya usajili tu wa kikosi chao, mimi natofautiana nao kidogo.

Kama Yanga inafikiri usajili wa kikosi chao ndio utawasaidia hilo halitawezekana kwani kwanza wanapaswa kufanya usajili wa uongozi wao kwa kuwa sioni kama wanaweza kufanya ulio sahihi kwa aina ya viongozi walionao sasa.

Matokeo ambayo viongozi wameyatoa kwa waliowapa dhamana yangetosha hata wao wenyewe kujitathimini kisha kuchukua hatua kwa kuwa wamejificha katika kivuli kimoja tu cha kazi ambayo imefanywa na mdhamini wao, GSM.

Ina maana kama isingekuwa hao timu ingendelea kuishi maisha ya tabu, kusafiri kwa hali ngumu na kushindana kichovu. Huu ni ukweli ingawa mchungu.

Busara kwa uongozi wa Yanga sasa ni kutoa mrejesho kwa wanachama wao wa kipi wamekifanya kwa zaidi ya mwaka mmoja ndani ya uongozi na sababu za kina za anguko hili ambalo limeshamaliza mwaka wa hasara kwa klabu yao.

Yanga inapaswa kujifunza kwa kiasi fulani safari ya Simba kwani uongozi wao mpaka kikosi chao wanaonekana kuwa katika utulivu mkubwa wakipanga mambo yao na sasa mafanikio yanaonekana kwa kuchukua mataji.

Yanga hali ni tofauti, kikosi chao tu kinaonekana na changamoto kubwa ya nidhamu na sasa mambo yameharibika zaidi hadi kufikia hatua ya makocha kutimuana.

Hakuwezi kukawa na mafanikio eneo hilo, ni muhimu sasa kwao kujipanga upya na kuamua kipi wanakihitaji kuporomoka zaidi au kujisuka upya.

Inawezekana wapo watu wa Yanga hawataki kukubaliana na mafanikio ya Simba, lakini itoshe kutambua kwamba inawezekana mafanikio ya Simba yametokana na kuyumba zaidi kwa uongozi wa klabu yao uliowafanya Wekundu wa Msimbazi hao kunuifaika na makosa wa yule anayewakimbiza.

Wakishamaliza kusuka uongozi sasa ndio wageukie kusuka benchi la ufundi ambalo nalo linaonekana kuyumba zaidi.

Baada ya hapo, sasa kazi ya kumalizia iwe kuunda kikosi chao tayari kwa msimu ujao, lakini kama wataruka kujisahaulisha kusuka uongozi sioni kama Yanga itaweza kuinuka kirahisi katika anguko ambalo imepitia kwa miaka mitatu.

Advertisement