Ka Mariga, Wanyama, Mourinho anahusika

Thursday November 21 2019

 

By Thomas Matiko

Nairobi, Kenya.UTEUZI wa Kocha Jose Mourinho kuwa mwalimu mpya wa klabu ya Tottenham Hotspurs Jumatano umeibua kumbukumbu za kiungo wake wa zamani ambaye sasa ni mstaafu McDonald Mariga.

Mourinho aliyeteuliwa kurithi mikoba yake Kocha Mauricio Pochettino aliyetimuliwa kazi kutokana na matokeo duni, anakumbukwa sana kwa namna alivyomjenga Mariga.

Kocha huyo  ndiye aliyemsajili Mariga 2010 akimtoa FC Parma na kisha kumtumia kwa muda akimfanya kuwa Mkenya wa kwanza kushiriki na kushinda taji la Champions League.

Miaka kumi baadaye, Mariga akiwa amestaafu soka na kujitosa kwenye siasa, Mourinho sasa kajipata akiwa na majukumu mapya ya kumfufua tena mdogo wake Mariga, Victor Wanyama ambaye amekuwa akihangaikia fomu yake kiasi kuwa kocha aliyefutwa tayari alikuwa ameshapoteza imani naye.

Hii ni licha ya Kocha Pochettino ndiye aliyemvuta Wanyama kutoka Celtic ya Scotland na kumleta Uingereza alipokuwa akiifuza Southampton. Pochettino alipohamia Tottenham, tena ndiye aliyemvuta Wanyama klabuni humo.

Wakati akiteuliwa kocha mpya, Wanyama ambaye ni nahodha wa timu ya taifa Harambee Stars ndio alikuwa ameondoka katika Uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta akiabiri pipa kurudi zake London, Uingereza kujiunga na klabu yake ya Tottneham.

Advertisement

Wanyama alikuwa na Stars kwa ajili ya mechi za kimataifa na aliwaongoza kutoka sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Misri na Togo kwenye mechi za kundi G kufuzu kwa hatua ya makundi ya AFCON 2021.

Uteuzi wa Mourinho huenda ukampa afueni Wanyama kutokana na mtazamo kocha huyo anafahamika sana kwa kupendelea michango ya wachezaji Waafrika uwanjani.

Advertisement