Mourinho haishiwi vituko

Friday November 9 2018

 

TURIN, ITALIA BAADA ya matusi mengi kutoka kwa mashabiki wa Juve majukwaani ndani ya dakika 90 za pambano la juzi Jumatano, kocha wa Manchester United, Jose Mourinho mwisho alicheka mwisho pale Turin na pambano lilipomalizika akawauliza, ‘Mnasema?’

United iliondoka na ushindi wa kufurahisha wa mabao 1-2 ugenini kwa Juventus juzi Jumatano usiku huku ikionekana kama vile ilikuwa inapoteza pambano hilo. Lakini mabao ya Juan Mata na bao la kujifunga la Leonardo Bonucci yalitosha kulifunika bao la Cristiano Ronaldo na kuipa United ushindi muhimu ugenini.

Mourinho amedai alikuwa ametukanwa muda wote na mashabiki wa Juventus huku mbaya zaidi wakimtukania familia yake, kitu ambacho kilisababisha mwishowe awasikilize vizuri zaidi walikuwa wanasemaje baada ya kuwachapa kwao.

“Nilitukanwa kwa dakika 90. Nafanya kazi yangu na sio kitu kingine. Mwishowe sikumtukana mtu yeyote yule. Nilitoa ishara tu kwamba nilitaka kuwasikia zaidi.

Sitafanya tena. Lakini nilikuja hapa kama mtu mwenye weledi na kazi yangu na watu wakaitukana familia yangu. Ndio maana nilijibu mapigo vile. Sitaki kufikiria hilo,” alisema Mourinho.

“Katika mji mzuri wa Italia, walinitukana kwa dakika 90. Sikuwatukana. Nilifanya kitu kidogo. Najua mamilioni ya mashabiki wa Inter wamefurahia sana. Lakini nawaheshimu Juventus, wachezaji wao, kocha wao, na ubora ambao wanao,” alisema Mourinho ambaye aliwahi kuwafundisha wapinzani wa Juventus, Inter Milan kati ya mwaka 2008 hadi 2010.

Mourinho aliongelea kuhusu ushindi huo ambao unawaacha katika nafasi ya pili wakiwa na pointi saba katika kundi lao la H. anaamini ushindi huo unalingana na ule wa kikosi cha, Sir Alex Ferguson wakati wakielekea kuchukua Ubingwa wa Ulaya mwaka 1999.

“Ni wazi wakati Manchester United inafanya ushujaa hapa (mara ya mwisho walipocheza nao) Manchester United ilikuwa timu bora na Juventus wamekuwa timu bora kwa miaka mingi sasa.

Walimnunua mchezaji yule (Ronaldo), wanataka kushinda kila kitu, wanaweza kushinda kila kitu. Sisi ni timu ambayo wachezaji wetu wengi hawajacheza mechi kubwa kama hizi za Ligi ya Mabingwa,” aliongeza Mourinho.

Hata hivyo, kitendo cha Mourinho kimemkera staa wa zamani wa Manchester United, Paul Scholes ambaye mara kwa mara amekuwa akimkalia kooni kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo kiwango cha timu yake.

Scholes anaamini Mourinho alipaswa kuwa muungwana mara baada ya kumalizika kwa pambano hilo hata kama ni kweli kuwa mashabiki wa Juventus walikuwa wanamtukana.

“Hivyo ndivyo alivyo kila anapokwenda. Inahitaji ushinde huku ukionyesha werevu wako. Unapeana mkono na kocha wa timu pinzani, unakwenda kuwapigia makofi mashabiki wako. Sidhani kama kuna umuhimu wa kufanya vile, lakini hivyo ndivyo alivyo,” alisema Scholes.

Hata hivyo, kocha huyo Mreno alitetewa na staa wa zamani wa United, Owen Hargreaves ambaye alidai labda kocha huyo alikuwa ameelewa na furaha kutokana na kuwa na ‘wiki nzuri’ klabuni hapo na kicheko chake kinaweza kueleweka.

“Haikuwa muhimu lakini ulikuwa ushindi mzuri sana. Ni wiki nzuri kwa United na Mourinho mwenyewe,” alisema staa huyo wa zamani wa kimataifa wa England ambaye naye kwa sasa ni mchambuzi kama ilivyo kwa Scholes.

Advertisement