KMC yawekea mtego mastaa wake

Muktasari:

KMC ilianza kushiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu wa 2018/2019 ambapo ilimaliza ikiwa katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi na msimu uliopita wa 2019/2020 imemaliza ikiwa katika nafasi ya 13

WAKATI vuguvugu la usajili likianza kupamba moto kwa kasi, timu ya KMC imepanga kutofanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake huku ikiwaweka mtegoni nyota wake wanaowaniwa na timu mbalimbali.

Akizungumza na Mwanaspoti Online, Meneja wa timu ya KMC, Faraji Muya amesema kuwa hawatarajii kufanya usajili mkubwa katika timu yao kwa sababu hawana mahitaji mengi.

"Mipango yetu ya usajili kwa ajili ya kuimarisha timu inaenda safi.Tunajaribu kufuata ripoti ya kocha na ya bodi ili kuziba mashimo ya wachezaji wanaotoka na mapungufu tuliyonayo.

"Kwa awamu hii hakuna atakayetemwa bali tutatafuta mbadala wa wachezaji ambao wataondoka," amesema Muya.

Katika hatua nyingine, KMC imeziweka wazi timu zenye nia ya kusajili wachezaji wake kuwa zisitegemee kuwapata bure kwa kuwa wengi wao wana mikataba ya muda mrefu ya kuitumikia timu hiyo.

Angalizo hilo la KMC limekuja baada ya uwepo wa taarifa za nyota wake, Charles Ilanfya, Kelvin Kijiri, Abdallah Mfuko na Hassan Kabunda kuwa kwenye rada za timu mbalimbali zinazoshiriki ligi hiyo.

"Uzuri sisi timu yetu kundi kubwa la wachezaji wana mikataba ya kuendelea kuichezea ni kama asilimia 70 hivyo kama kuna wanaowahitaji wafuate utaratibu waje mezani," aliongeza meneja huyo.