KMC yaipapasa Ruvu Shooting ya Masau Bwire

Muktasari:

Mchezo huu ni muendelezo wa mzunguko wa pili unaoendelea licha ya kwamba timu zingine zipo Zanzibar zikicheza kombe la Mapinduzi Cup.

KIKOSI cha KMC kinachonolewa na Ettiene Nayiragije kimeibuka na ushindi 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Uhuru.
Mchezo huu ni muendelezo wa mzunguko wa pili unaoendelea licha ya kwamba timu zingine zipo Zanzibar zikicheza kombe la Mapinduzi Cup.
Katika kipindi cha kwanza timu zote zilikuwa zikitengeneza nafasi nyingi lakini kwenye upande wa kumalizia kote walionekana kusua sua.
Upande wa Ruvu Shooting kwenye eneo la ushambuliaji Said Dilunga alionekana kutokuwa na msaada kiasi cha kumfanya ashindwe kufanya kazi yake vizuri.
Mshambuliaji huyo mwenye magoli 10 chini ya Herieter Makambo mwenye 11, hakuweza kabisa kutamba mbele ya mabeki wa KMC wakiongozwa na Yusuph Ndikumana.
Katika upande wa KMC pengo la Elius Maguli na James Msuva lilionekana kwani walikuwa wakitengeneza nafasi nyingi lakini hata hi yo walishindwa kutumia.
Dakika 48 Cliff Buyoya aliingia kuchukua nafasi ya Masoud Abdallah, mabadiliko hayo yalizaa matunda kwani dakika 65 Cliff aliiandikia bao la kuongoza KMC.
Baada ya kupata bao hilo KMC walizidi kucharuka kutengeneza nafasi lakini hata hivyo mshambuliaji wao Mohammed Rashid alionekana kutokuwa vizuri katika umaliziaji.
Mabadiliko ya Shooting kwa kumtoa Dilunga na kuingia Full Maganga bado hayakuonyesha tija katika kikosi chao.