KMC, Coastal Union wagawana pointi

MECHI ya Ligi Kuu Bara kati ya KMC dhidi ya Coastal Union uliochezwa katika Uwanja wa Uhuru jioni ya leo umemalizika kwa suluhu na timu zote mbili kugawana pointi moja moja.

 

Baada ya kugawana pointi hizo KMC watakuwa wamefikisha pointi kumi wakipanda mpaka nafasi ya nne ila wakiwa mbele kwa mchezo mmoja huku wakiwa wamecheza mechi sita, wakishinda tatu, wametoka sare mbili na kufungwa moja wakiwa wamefunga mabao nane na wao kufungwa manne.

 

Coastal Union baada ya matokeo hayo wamefikisha pointi tano na kupanda mpaka nafasi ya kumi wakiwa wamecheza mechi sita, wameshinda moja wametoka sare mbili, wamefungwa tatu huku wakiwa wamefunga bao moja na wao kufungwa sita.

 

Baada ya kipindi cha kwanza KMC beki wake wa kulia Ally Ramadhani kupewa kadi nyekundu katika kipindi cha pili waliingia na malengo ya kuzuia zaidi na kufanya mashambulizi machache ya kushtukiza.

 

Ukiondoa nafasi tatu ambazo KMC walipata kipindi cha kwanza kupitia Raliants Lusajo, Hassan Kabunda na Emmanuel Mvuyekule katika kipindi cha pili hawakuonekana kushambulia zaidi kutokana na kupungua kwa mchezaji mmoaj.

 

Union wao walionekana kukosa plani katika kutengeneza nafasi za kufunga kwani walifika muda mwingi katika lango la KMC lakini mashuti na mashambulizi yao mengi yalionekana kupotea kwa kuzuia na walinzi wa KMC.

 

Namungo nao wamepata ushindi wa tatu wakiifunga Kagera Sugar mabao 2-1 wakati wakifungwa mechi tatu huku Biashara United waliorudi kwenye uwanja wao wa nyumbani Mara wameshinda bao 1-0 dhidi ya Ihefu lililofungwa na Hamadi Tajiri dakika ya 87 na mechi nyingine ilikuwa JKT Tanzania 0-1 Ruvu Shooting