KAKOLANYA : Huu ndo’ ukweli mimi kusaini Simba - 2

Muktasari:

  • KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya na kipa Beno Kakolanya, tuliona jinsi anavyosotea kesi yake iliyopo katika Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji akipigania aachwe huru katika mkataba wake na Yanga akiwatuhumu kuuvunja kwa kutomlipa malimbikizo ya mshahara wake. Twende pamoja katika sehemu hii ya mwisho:

KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya na kipa Beno Kakolanya, tuliona jinsi anavyosotea kesi yake iliyopo katika Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji akipigania aachwe huru katika mkataba wake na Yanga akiwatuhumu kuuvunja kwa kutomlipa malimbikizo ya mshahara wake. Twende pamoja katika sehemu hii ya mwisho:

AMVULIA KOFIA KASEJA

Ni ngumu mchezaji wa Kitanzania kumsifia hadharani mchezaji mwenzake anayekipiga naye Ligi Kuu, lakini kwa Kakolanya ni tofauti kwani bila kuficha anaweka wazi tangu utotoni mwake alikuwa akivutiwa na uwezo wa kipa, Juma Kaseja.

“Kaseja tangu nikiwa mtoto nilikuwa namkubali kwa hawa wanaocheza ligi ya ndani, anajiamini anapokuwa yupo uwanjani na anatambua umuhimu wa kazi yake, lakini kwa nje namkubali Iker Casillas anavyocheza.”

Aliongeza anaamini kipa huyo amedumu muda mrefu katika soka la Bongo kutokana na kufanya mazoezi na kuzingatia misingi ya mchezaji anavyotakiwa kuishi.

MCHELE WAENDESHA MAISHA YAKE

Kukaa nje zaidi ya miezi minne huku ukiwa unategemea mpira siyo jambo dogo kabisa.

Yanga waliacha kumWingizia mishahara baada ya yeye kujiweka pembeni hivyo jamaa akajiongeza kwa kujikita katika biashara ya kuuza mchele.

Mwenyewe anafunguka biashara hiyo imekuwa ikiendesha maisha yake ya kila siku licha ya kukaa nje ya uwanja, hivyo anaamini kabisa atazidi kujitanua katika biashara hata kama akirejea uwanjani.

“Nafanya biashara ndogondogo ikiwamo hii ya mchele, nauza kwa watu mbalimbali na muda mwingine huwa nawapelekea mimi mwenyewe mpaka nyumbani pindi wanapopiga simu, nashukuru Mungu maisha yanayoendelea.”

MALENGO HAYAJATIMIA

Wachezaji wanaotoka katika timu ndogo na kusajiliwa Simba na Yanga, wengi huona kama wameshatimiza ndoto zao, lakini kwa Kakolanya ni tofauti.

Kakolanya alisema ndoto yake ilikuwa siyo kucheza Yanga pekee kwa sababu anaamini bado ana umri mdogo hivyo ilikuwa ni njia kwake ya kutafuta maisha.

“Yanga ni timu kubwa ambayo kila mchezaji nchini lazima atamani kuwa miongoni mwa wachezaji waliocheza pale, nimeishi nao vizuri sana najivunia hilo kwa wachezaji wenzangu, lakini bado nina safari ndefu ya kuendelea kutafuta maisha yangu.”

Aliongeza kuigomea Yanga siyo kama ameshindwa kulipa fadhila za klabu hiyo iliyomvumilia kipindi anaumwa, lakini walikuja kutofautiana katika makubaliano waliyoweka na baadhi ya viongozi.

DILI SIMBA, AZAM

Kumekuwa na tetesi ambazo zinaibuka kadri siku zinavyozidi kwenda mbele kwamba kipa huyu amesaini makubaliano ya awali ya kujiunga na Simba au Azam kwaajili ya msimu ujao.

Hata hivyo, mwenyewe anasema hakuna kiongozi ambaye amemfuata na kukaa naye chini kuzungumzia dili hilo, pia anasubiri kuona mambo yake yanaendaje kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji.

“Hizo ni tetesi tu zinazungumzwa na muda mwingine hata mimi ninapokuwa nazisikia huwa nashangaa, nawezaje kusaini na klabu nyingine ikiwa kesi yangu haijaisha? Ninasubiri kuona kwanza kesi yangu inaishaje halafu ndiyo nitajua hatma yangu ipoje,” alisema.

NDOTO YA UJEDA

Kama ilivyokuwa kwa wachezaji wengi hapo awali kuwa na ndoto mbalimbali mbali, basi kwa Kakolanya napo ilikuwa hivyo hivyo kwani alikuwa na ndoto tofauti na soka.

Aliliambia Mwanaspoti kama isingekuwa soka basi angevaa gwanda kwa vile alikuwa anatamani siku moja awe mwanajeshi lakini baadaye ndoto hizo zilifutika kutokana na kuzidi kujitanua katika soka.

“Nilikuwa nataka niwe mwanajeshi lakini baadaye ndoto hiyo ilipotea hasa baada ya kutua Yanga.“

MANULA KIBOKO

Kakolanya alikitaja kikosi chake bora cha msimu huu na hakuacha kumtaja kipa mwenzake wa timu ya Taifa na klabu ya Simba, Aishi Manula.

Kikosi chake chake cha wachezaji bora wa Ligi Kuu ya Bara msimu huu anawataja: Aishi Manula, Paul Godfrey ‘Boxer’, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, James Kotei, Clatous Chama, Feisal Salum ‘Fey Toto’, Meddie Kagere, Heritier Makambo na John Bocco.

Anasema siyo kama wachezaji wengine hawafanyi vizuri, lakini ameangalia kwa upande wake kwa jinsi ambavyo wachezaji hao wamecheza kwa msimu huu.