Julio hatua ya mtoano iangaliwe upya

Muktasari:

  • Klabu za Ligi Kuu Kagera Sugar na Mwadui kunusurika kubaki Ligi Kuu Bara baada ya kupata ushindi katika mechi zao za mwisho za hatua ya mtoano (Playoff) shisi ya Pamba na Geita Gold.

Dar es Salaam. Kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo 'Julio' amesema mfumo wa playoff unatakiwa kuangaliwa upya kwani kuna jambo halipo sawa.

Kauli hiyo ya Julio inatokana na klabu za Ligi Kuu Kagera Sugar na Mwadui kunusurika kubaki Ligi Kuu Bara baada ya kupata ushindi katika mechi zao za mwisho za hatua ya mtoano (Playoff).

Kagera Sugar walimfunga Pamba mabao 2-0, wakati Mwadui alimfunga Geita mabao 2-1, huku mechi za mzunguko wa kwanza zote mbili zilimalizika kwa suluhu.

Julio alisema mchakato wa Playoff si mbaya ila kuchezwa ilitakiwa kama ni timu za Ligi Kuu Bara zicheze zenyewe au kama za Ligi daraja la kwanza iwe hivyo hivyo.

"Kama wakiendelea kucheza playoff kwa maana ya timu za Ligi Kuu Bara na Ligi daraja la kwanza haitakuwa siyo sawa kwani tunachezesha timu zenye madaraja mawili tofauti," alisema Julio.

"Miaka yote hii playoff isipo angaliwa na kubadilishwa timu za Ligi Kuu Bara hakuna hata moja ambayo itashuka na kwenda Ligi daraja la kwanza kwani zenyewe zinauwezo katika maeneo mengi kuliko wapinzani wao.

"Kwangu nilitamani kuona timu za Ligi Kuu Bara zote nne zitakazoshika nafasi ya chini zishuke na mbili zitakazo ongoza makundi ya Ligi darala la kwanza zipande na zitafutwe mbili nyingine kucheza playoff zenyewe kwa zenyewe," alisema Julio.