Jose Mourinho anasa jembe la Spurs

Muktasari:

Spurs ndoto zao za kuifukuzia Top Four zimekabiliana na changamoto nyingi wakishinda mara moja tu katika mechi tano za mwisho walizocheza kwenye ligi.

LONDON, ENGLAND.JOSE Mourinho amefanya usajili wake wa kwanza huko Tottenham Hotspur baada ya kumnasa Gedson Fernandes kwa mkopo wa miezi 18. Mourinho amemnasa mchezaji huyo kutoka Benfica na kuweka makubaliano ya kumnunua kwa Pauni 45 milioni kama watafurahishwa na huduma yake.

Baada ya kusaini tu, Gedson alisema: “Kila mchezaji anapenda kuja kucheza kwenye Ligi Kuu England na hili kwangu ni ndoto zilizotimia. Nakijua kikosi cha Spurs kwa sababu nimekuwa nikitazama mechi zao. Namjua Sissoko na Eric Dier kwa sababu alicheza Ureno.

“Wachezaji wote vijana wanapenda kufanya kazi chini ya Jose Mourinho kwa sabbu ni kocha bora, mtu safi.” Gedson, atavaa jezi namba 30 huko Spurs na mwenyewe amejiwekea mipango ya kufika mbali kwenye kikosi hicho licha ya kuonekana si kitu kwa msimu huu huko Benfica.

Spurs ndoto zao za kuifukuzia Top Four zimekabiliana na changamoto nyingi wakishinda mara moja tu katika mechi tano za mwisho walizocheza kwenye ligi. Mourinho ameshatumia Pauni 138 milioni kunasa wachezaji wa kutoka Benfica wakiwamo Angel Di Maria, Victor Lindelof, Nemanja Matic na Fabio Coentrao kwa kuwataja kwa uchache.