Javu ajiapiza Alliance haishuki daraja

Muktasari:

  • Javu tayari ameshatupia mabao mawili na kuisaidia Alliance kuvuna pointi 24 na kukaa nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Mwanza. Mshambuliaji wa Alliance FC, Hussein Javu amesema kutokana na mwenendo wao ulivyo katika Ligi Kuu kuna kila sababu ya timu hiyo kufanya vizuri na kukwepa rungu la kushuka daraja.

Javu aliwahi kutamba na Yanga alijiunga na Alliance kwa kipindi cha dirisha dogo akitokea Mtibwa Sugar,ambapo hadi sasa ameshafunga mabao mawili likiwamo moja la kombe la Shirikisho.

Javu alisema haoni tatizo lolote litalowakwamisha kupata matokeo mazuri na kwamba ishu ya kushuka daraja kwa timu hiyo, haipo.

Alisema kuwa kwanza anafurahia kwa kombinesheni yao inayoundwa na Bigirimana Braise na Dickson Ambundo ambayo kwa mechi walizocheza wamepata matokeo mazuri.

“Kwanza nafurahia mazingira kwa sababu tangu niwasili nimepata nafasi ya kucheza, lakini niwaambie wadau wasahau ishu ya Alliance kushuka daraja, kombinesheni yetu ni hatari na mechi tulizocheza tumepata matokeo mazuri,” alisema Mkongwe huyo.

Hata hivyo Mshambuliaji huyo hakusita kuweka wazi ugumu wa Ligi kwa jinsi kila timu inavyopambana kusaka ushindi na kusema kuwa hilo linawapa shaka kuhakikisha wanakaza ili kufikia malengo yao.

Kuhusu ufungaji bora katika msimu huu, mkongwe huyo alisema kuwa lolote linawezekana kwani mechi zilizobaki akibahatika anaweza kufunga mabao mengi na kutwaa tuzo hiyo kwani kikosi chao kina ushirikiano.

“Ligi ni ngumu kila timu unaona inavyopambana kusaka ushindi popote, kwahiyo na sisi Alliance inatupa shaka kuhakikisha tunaongeza juhudi kutafuta pointi tatu, naweza kutwaa tuzo ya mfungaji bora kikubwa ni kujituma,” alisema Javu.