James Rodriguez kuleta vita kali Big Six

Saturday November 9 2019

 

MADRID, HISPANIA . VITA kubwa itaibuka kuwahusu vigogo wa Big Six kwenye Ligi Kuu England kuhusiana na huduma ya kiungo anayetendewa vibaya huko Real Madrid, James Rodriguez.

Staa huyo wa kimataifa wa Colombia, amemaliza muda wake wa mkopo huko Bayern Munich na kurudi kwenye timu yake ya Real Madrid, mahali ambako mambo yamekuwa sio mambo kutokana na Kocha Zinedine Zidane kumpiga tu benchi huko Santiago Bernabeu.

Rodriguez kwa sasa ameonekana kufanya uamuzi akitaka kuachana na Madrid kwenye dirisha la Januari huku akitaka kwenda kupiga kazi kwenye Ligi Kuu England. Jambo hilo linazifanya Chelsea, Arsenal na Manchester United kuripotiwa kuingia kwenye vita kali ya kunasa saini yake.

Kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi, mabosi wa Real Madrid walikuwa tayari kumruhusu kwenda Napoli, lakini jambo hilo lilikwama na mchezaji huyo aliendelea kubaki katika kikosi hicho cha Zidane.

Man United ilifeli kwenye mpango wake wa kusajili kiungo kwenye dirisha lililopita baada ya kuwakosa Bruno Fernandes na Christian Eriksen, lakini sasa Januari inaweza kugeukia kwa Rodriguez kuja kumaliza tatizo la ubunifu kwenye kikosi hicho cha Old Trafford. Chelsea na Arsenal nazo zinamfuatilia kwa karibu kabisa staa huyo sambamba na mabingwa wa Italia, Juventus.

Advertisement