Jahazi la Mbeya City lazidi kuzama

JINAMIZI la matokeo mabaya limeendelea kuiandama Mbeya City katika Ligi Kuu msimu huu baada ya leo kulazimishwa sare tasa na Dodoma Jiji FC katika mechi iliyochezwa katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.

 

Baada ya kupata pointi moja katika mechi tano ilizocheza dhidi ya timu za Yanga, KMC, Namungo, Prisons na Azam ilitegemewa pengine leo wangepata ushindi wa kwanza msimu huu mbele ya Dodoma Jiji ugenini lakini mambo yameendelea kuwa magumu kwa kupata sare ambayo imewafanya waendelee kubakia mkiani wakiwa na pointi zao mbili.

 

Matokeo hayo sio tu yamewafanya wabakie chini bali pia yamewafanya waandike rekodi ya kuwa timu iliyocheza idadi kubwa ya mechi mfululizo za mwanzoni za ligi bila kufunga bao ambapo wamefanya hivyo katika mechi zote sita walizocheza.

 

 

 

Kwa upande mwingine, matokeo hayo, yanawafanya Dodoma Jiji, kufikisha pointi 11 na imepanda nafasi kwa mbili katika msimamo wa ligi kutoka ya saba hadi ya tano na kuzishusha Polisi Tanzania na KMC.

 

Mbeya City, mchezo unaofuata itaikabili Mwadui FC ambayo jana ilipoteza kwa kipigo cha mabao 3-0 mbele ya Azam FC, mechi iliyopangwa kuchezwa Oktoba 20,

 

Straika wa Dodoma Jiji, Peter Mapunda ambaye alikuwa straika wa zamani wa Mbeya City, amesema mechi ya leo ilikuwa na ushindani, lakini wanashukuru hawajapoteza.

 

"Pamoja na kwamba Mbeya City, haijafunga bao hata katika mechi moja kati ya sita ambazo wamecheza, mchezo ulikuwa mgumu ndio maana tumeambulia suluhu tukiwa nyumbani,"amesema.