JKT Tanzania wala hawana mpango

Muktasari:

Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Abdallah Mohammed 'Bares' amesema, hafikirii kusajili mchezaji mpya katika kipindi cha dirisha dogo.

KOCHA Mkuu wa JKT Tanzania, Abdallah Mohammed 'Bares' amesema, hafikirii kuongeza mchezaji mpya ndani ya kikosi chake katika kipindi cha dirisha dogo la usajili, unaotarajiwa kuanza Novemba 15 hadi Desemba 15.
Amesema, anaweza kufanya hivyo, endapo wachezaji alionao kama wataondoka kwenda timu nyingine kwa ajili ya kuziba mapengo yao.
Kocha huyo ambaye kwa sasa kikosi chake kinashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wenye timu 20, ikiwa na pointi 12 walizopata katika mechi tisa.
"Katika usajili wa dirisha dogo, sifirii kabisa kuongeza mchezaji kwenye timu yangu kwa sababu hawa nilionao nataka kukaa nao kwa kipindi kirefu kwa sasa ni mapema kusema nawatoa,"alisema Bares.
"Naweza kusajili kama baadhi yao wataamua wenyewe kuondoka. Si unajua kuna timu zenye pesa huwa zinapanda dau, ikiwa hivyo nitakuwa sina jinsi."
Hata hivyo, kwa sasa Ligi Kuu ipo kwenye mapumziko  kupisha mechi za timu ya Taifa Stars na inatarajiwa kutimua vumbi tena Novemba 23 ambapo maafande hao wanatarajiwa kuwa wageni wa Yanga kwenye Uwanja wa Uhuru.
Dirisha dogo la usajili wa dirisha dogo unatarajiwa kuanza Novemba 15 na utamalizika Desemba 15.