JICHO LA MWEWE: Usishangae sana Yanga inapokaa kileleni kihuni

Muktasari:

Unajua kwanini ipo kileleni huku wachezaji wakiwa hawana mishahara? Sijui hizi timu kubwa zilijiunda vipi wakati huo zikiundwa. Lakini Yanga ni timu ya wananchi. Mashabiki wake ni raia wa kawaida kabisa. Wengi wengi kati yao ni walalahoi na wanaipenda timu yao kupindukia.

USISHANGAE sana Yanga kuwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu huku wachezaji wakiwa hawana mishahara. Wana kauli yao inasema ‘Daima mbele nyuma mwiko’. Wakati mwingine Yanga inanikosha sana nje ya uwanja.

Unajua kwanini ipo kileleni huku wachezaji wakiwa hawana mishahara? Sijui hizi timu kubwa zilijiunda vipi wakati huo zikiundwa. Lakini Yanga ni timu ya wananchi. Mashabiki wake ni raia wa kawaida kabisa. Wengi wengi kati yao ni walalahoi na wanaipenda timu yao kupindukia.

Mapenzi yao yanatoa presha kubwa kwa wachezaji. Popote wanapokwenda, hata kama timu yao inapitia kipindi kibovu, Yanga itapokewa na maelfu ya mashabiki huku wengi kati yao wakiwa ni walalahoi. Hapo hapo wachezaji wanapata ari ya kupambana.

Juzi nimeona wametua Mbeya, mashabiki wakajipanga katika mistari miwili kuipokea timu yao. Nilicheka sana nikakumbuka tabia za Yanga. Hilo limetokea wakati timu haina fedha. Hiyo ni janja ya mashabiki kuwatia morali wachezaji. Mbona wakati wana pesa hawajawahi kuwapokea kwa staili ile?

Wakiwa katika Uwanja wa Taifa, wachezaji wa Yanga wanakuwa na wakati mgumu zaidi. Mashabiki wana mahitaji makubwa zaidi. Wanawataka washinde mechi bila ya kujali kama wachezaji hawajala, wamelala sehemu mbovu, hawana mishahara na mengineyo.

Kule kwa watani zao mara nyingi timu ikifungwa huwa wanalalamikiwa viongozi au makocha. Wachezaji wanabakia salama. Jiulize, ni kitu kilisababisha hadi Haji Manara atupiwe chupa za maji baada ya timu kupoteza mechi ya Mbao FC? Haji ni msemaji tu wala sio mchezaji.

Kwa Yanga, Deus Kaseke amewahi kupigwa na shabiki. Simon Msuva pia amewahi kupigwa na shabiki. Zamani Athuman China aliwahi kutiana ngumi na shabiki vilevile. Mahitaji ya mashabiki wa Yanga ni makubwa kuliko mahitaji ya mashabiki wa Simba.

Simba ina kaustaarbu fulani hivi. Wanaweza kupoteza mechi wakalalamika chinichini wakaenda kulala. Kwa Yanga haiwezekani. Lazima mashabiki waendeshe mashtaka nje ya Uwanja wa Taifa, wajipe ushahidi kisha watoe hukumu. Wakati mwingine hukumu inakuwa mbaya kwa wachezaji.

Wakati mwingine unajiuliza, kwanini kwa miaka nenda rudi, Yanga huwa inapata wachezaji wanaojituma sana halafu wakati mwingine Simba inaonekana inapata wachezaji mabishoo. Tangu enzi za kina Hussein Marsha. Kuna mchezaji anajulikana huyu amekaa Kisimbasimba na yule amekaa Kiyangayanga.

Mchezaji mwenye mbio, anayepambana sana uwanjani, anajulikana kama ni wa Yanga. Mchezaji fundi, mtaratibu asiye na haraka sana anajulikana kuwa mchezaji wa Simba. Wengine wanadai Mtemi Ramadhani asingeweza kucheza Yanga. Kama ambavyo wengine wanadai mchezaji wa aina ya Edibily Lunyamila amekaa Kiyanga zaidi.

Aina hii ya wachezaji huwasaidia sana Yanga wakati wa matatizo. Yanga daima watapambana tu, kuwe na njaa au shibe. Simba kidogo huwa wanapata wakati mgumu kupambana wakati wa njaa. Labda kwa sababu ya aina yao ya wachezaji, au kwa sababu hawana presha kubwa nje ya uwanja.

Na wakati mwingine inashangaza kuona wachezaji wa Yanga wanarithishwa kuipenda zaidi klabu yao hata wanapoacha soka. Kwa mfano, mara nyingi ukienda Uwanja wa Taifa unakutana na wachezaji wengi wa zamani wa Yanga kuliko wa Simba.

Ukienda mechi za Yanga, hasa zile ngumu unakutana na kina Lunyamila, Mohamed Hussein, Makumbi Juma, Mwanamtwa Kihwelo, Abuubakar Salum na wengineo. Ukienda mechi za Simba ni nadra kukutana na wachezaji wao wa zamani.

Hata katika uchaguzi, wachezaji wa zamani wa Yanga ama wanagombea, au wanakuwa karibu na fitina za uchaguzi. Ni tofauti na wale wa Simba ambao licha ya kuifuatilia klabu yao kwa karibu lakini mara nyingi wanajikuta wamejiweka mbali na fitina za klabu yao.

Wakati mwingine hata ukifuatilia inakuwa ngumu sana kwa wachezaji wanaohama Yanga kwenda Simba kutamba wakiwa na jezi za Msimbazi. Lakini kwa muda mrefu wachezaji wanaotoka Simba kwenda Yanga wanang’ara na wanaendelea kuwa tegemeo katika timu.

Mfano wa karibuni ni Ibrahim Ajib. Anaendelea kutamba na Yanga baada ya kuhamia akitokea Simba. Lakini maisha yamekuwa magumu kwa Haruna Niyonzima aliyetoka Yanga kwenda Simba. Inatokana na sababu nyingi mbalimbali lakini wakati mwingine mashabiki wa Simba wanaweza kuachana na habari za mchezaji wao aliyehamia Yanga na maisha yakaendelea. Yanga huwa hawasemei.