JICHO LA MWEWE: Kinachomkumba Francis Kahata Simba hiki hapa!

SIMBA leo inacheza mechi yake ya raundi ya saba ya Ligi Kuu bila ya mashabiki kumuona kiungo Francis Kahata uwanjani. Kahata ni fundi kweli kweli lakini anaishia benchi. Hata katika pambano la majuzi dhidi ya Tanzania Prisons aliishia benchi.

Simba isiyo na Clatous Chama wala washambuliaji wake, John Bocco, Meddie Kagere na Chris Mugalu, lakini bado Kahata alijikuta akisugua benchi pale Sumbawanga. Inasikitisha ila ndio hali halisi. Nini kinamsibu Kahata?

Simba wana wachezaji wengi katika eneo lake. Wakati mashabiki wa Simba wakitanabaisha Simba ina kikosi kipana, ukweli ni kwamba katika eneo la viungo washambuliaji Simba inao wengi zaidi kuliko eneo lolote lile uwanjani.

Ni eneo hilo ukijumlisha na mawinga ndipo unapogundua Simba ina wachezaji zaidi ya saba katika eneo moja. Kuna Luis Miquissone, Hassan Dilunga, Ibrahim Ajibu, Chama, Miraji Athuman, wameongezeka Larry Bwalya na Bernard Morrison pia katika eneo hilo, halafu mjumlishe na Kahata mwenyewe.

Walioharibu zaidi ni Larry Bwalya na Morrison wanaolazimika kucheza eneo hilo ama wakitokea pembeni au katikati. Kahata amejikuta hana nafasi kabisa.

Nje ya hilo kuna kitu kimoja ambacho kitawagharimu Simba na kikosi chao kipana. Kitu ambacho kinamgharimu pia Kahata. Tanzania hatuna michuano mingi ya ndani. Wale watu waliotutawala, Waingereza, wana michuano mingi ambayo nadhani ingeweza kusababisha tumuone Kahata uwanjani.

Waingereza kwa ndani wana michuano mitatu ya Ligi Kuu, FA na Kombe la Ligi maarufu kama Carabao Cup. Kuna timu pia zinashiriki Ligi ya Mabingwa au michuano ya Europa. Wachezaji wanajikuta wanaweza kucheza mechi nyingi.

Kwa mfano, kuna wakati kocha wa Manchester City alikuwa na kikosi chenye wachezaji wawili mahiri katika kila nafasi. Kushoto walikuwepo Raheem Sterling na Leroy Sane. Kulia walikuwepo Bernardo Silva na Riyad Mahrez. Katikati walikuwepo Gabriel Jesus na Sergio Aguero. Nyuma yao walikuwepo Kelvin De Bruyne na David Silva.

Michuano minne ambayo City walikuwa wakishiriki ilikuwa inampa nafasi Guardiola kukipangua kikosi chake kadri alivyojisikia. Leo katika Ligi angeweza kuanza na Sterling kushoto, Jesus katikati, Mahrez kulia na nyuma yao angecheza De Bruyne.

Jumanne katika pambano la Ligi ya Mabingwa nje ya jiji la Manchester au ndani angeweza kuwapanga Sane kushoto, Aguero katikati, Bernardo Silva kulia na nyuma yao angecheza David Silva. Kilikuwa kitu cha kawaida tu.

Tatizo la Simba ni kwamba inashiriki Ligi Kuu ya Tanzania tu basi. Michuano ya FA haijaanza. Lakini hapo hapo kumbuka hatuna michuano ya aina ya Carabao. Hapo hapo kumbuka kwamba Simba haijacheza mechi ya michuano ya kimataifa tangu ilipotolewa na UD Songo mapema mwaka huu.

Pambano pekee ambalo Simba walicheza baadaye lilikuwa la kirafiki dhidi ya Vital’O ya Burundi katika tamasha lao la kila mwaka la Simba Day. Na sasa wamerudi katika Ligi Kuu huku wakishindwa kuwatumia wachezaji wote ipasavyo.

Matokeo yake Simba inawaacha wachezaji wengi nje. Ninachokiona ni kwamba muda si mrefu mchezaji kama Kahata ataomba kuondoka klabuni. Hauwezi kuwalaumu sana Simba wala haiwezi kumlaumu mchezaji mwenyewe.

Kahata anacheza katika timu ya taifa ya Kenya na ni wazi kwamba makocha wa timu za taifa, kama ilivyo kwa kocha wetu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije huwa wanafuatilia kwa karibu maendeleo ya mchezaji mmoja mmoja wa timu zao.

Kwa muundo wa soka letu kupitia kwa wachezaji kama Kahata na Ajibu imegundulika kwamba inawezekana hatuna mahitaji sana ya kikosi kipana. Ni ngumu kuwaridhisha wachezaji wote kwa kutumia michuano ya Ligi Kuu tu.

Matokeo yake wachezaji kama kina Kahata wanaweza kukimbilia timu nyingine kama Yanga na Azam wakawa mastaa wakubwa tu. Ilitokea kwa Ajibu alipokwenda Yanga na kuwa staa mkubwa. Amerudi Simba na anaonekana kama mchezaji wa kawaida. Mechi za kirafiki ambazo wamekuwa wakicheza asubuhi haziwezi kuzingatiwa na makocha wa timu zao za taifa.