JICHO LA MWEWE : Dilunga na maswali tata Simba

Muktasari:

  • Ilimchukua kutoka wapi? Lipuli ya Iringa. Alikuwa mshambuliaji tishio msimu uliopita na Simba haikutaka kufanya makosa. Wikiendi hii iliyoisha, Lipuli ilicheza Simba Dar es Salaam. Ni wazi Simba ilikuwa inaongezeka nguvu mara mbili dhidi ya Lipuli.

ADAM Salamba alikuwa miongoni mwa mastaa wa kwanza kutua Simba katika dirisha kubwa lililopita. Simba ilitengeneza kikosi cha mauaji. Tayari ilishakuwa na kikosi cha mauji lakini ilikuwa inataka kufanya mauaji zaidi msimu huu.

Ilimchukua kutoka wapi? Lipuli ya Iringa. Alikuwa mshambuliaji tishio msimu uliopita na Simba haikutaka kufanya makosa. Wikiendi hii iliyoisha, Lipuli ilicheza Simba Dar es Salaam. Ni wazi Simba ilikuwa inaongezeka nguvu mara mbili dhidi ya Lipuli.

Kwanza kabisa Simba ilikuwa imeimega Lipuli, pili ilijijenga zaidi. Hata hivyo, kilichotokea wakati wa mapumziko watu hawakuamini. Mchezaji staa wa Simba, Hassan Dilunga pamoja na mchezaji mwingine wa Lipuli waligoma kutoka uwanjani wakati wa mapumziko.

Nadhani maagizo ya waganga wao yalikuwa lazima mchezaji wa timu husika awe wa mwisho kutoka uwanjani. Ni tukio la kishirikina lililochukua dakika kadhaa. Likavuta hisia za wengi. Bado tupo katika zama hizi? Ajabu.

Sitaki kuizungumzia Lipuli. Kwao kucheza na Simba ni fainali. Kwao kuifunga Simba ni ndoto. Inaweza kufanya kila inachofanya kuifunga Simba, hata kutumia mlango wa uani kwa sababu inafahamu haiko katika kiwango sawa na SImba.

Nataka kuizungumzia Simba. Dilunga ametukumbusha yale maswali maarufu ambayo huwa tunajiuliza kuhusu Simba na Yanga. Wana haja ya kununua mastaa wa gharama kutoka nje kama wanategemea mganga? Wana haja gani ya kuleta makocha wa gharama kutoka nje? Wana haja gani ya kulipa mishahara mikubwa kwa mastaa wao?

Kwa jinsi ambavyo Simba imejiunda katika kipindi cha miezi 24 iliyopita nilidhani ina uwezo wa kuifunga Lipuli katika uwanja wowote wa soka bila ya kutegemea habari za waganga na maagizo yao. Nilijidanganya sana. Kumbe kuna utamaduni lazima uendelee.

Bado kuna watu wengi wanaoitwa Waganga ambao wamekuwa wakipata pesa nyingi kuliko kina Meddy Kagere. Ni suala la saikolojia kwa timu. Basi. Mbaya zaidi inafika mahala ambapo mchezaji mwenye kipaji kama Dilunga naye anaamini.

Ukitazama mageuzi ambayo Simba inajaribu kuyafanya, halafu katikati ya mageuzi hayo ambayo mashabiki wanaamini Simba itakuwa timu ya kisasa, lakini bado wachezaji wanaingia uwanjani wakiwa wamepewa maelekezo ya kishirikina. Aibu iliyoje.

Tukiachana na hilo, pamoja na uhodari wa wachezaji mastaa, kocha wa kigeni, timu hizi kubwa hujaribu kumuona mwamuzi au wachezaji wa timu pinzani kwa ajili ya kuifanya mechi kuwa nyepesi. Hapa ndipo unapogundua tumekwama kama taifa.

Hatuamini katika sayansi ya soka. Wachezaji wanaolipwa pesa nyingi kwa kufanya kazi yao wanazidi kuwa wazembe kwa sababu wanaamini kazi yao itarahisishwa katika mazingira mengine tofauti na uwezo wao ulivyo. Aibu iliyoje.

Sitaki TFF ichukue hatua yoyote kwa wachezaji waliohusika wala timu zao. Ni suala la timu zenyewe, hasa Simba kujitathmini kama ipo katika mwelekeo sahihi linapokuja suala la kile kilichotokea katika mechi dhidi ya Lipuli.

Sijui mwekezaji wake anakuja na malengo gani lakini ni wazi hawezi kukubali kukiona alichokiona. Sidhani kama kuna mwekezaji anaweza kununua wachezaji kwa bei mbaya, akalipwa kocha wa kigeni bei mbaya, akatengeneza viwanja vya mazoezi, akaajiri wataalamu halafu bado Dilunga akachelewa kutoka uwanjani wakati wa mapumziko kwa kusikiliza maelekezo ya waganga.

Ni mwekezaji wa ajabu anayeweza kukubali jambo hilo na ndio maana nataka Simba kama Simba ijitathimini.

Kuonyesha jinsi gani ambavyo tunajikanganya wenyewe katika suala la ushirikina ni kwamba mara zote ambazo Simba haijafanya vizuri imekuwa wakilaumiwa wachezaji au kocha.

Kwanini kocha wa sasa alitupiwa mawe Mwanza katika mechi dhidi ya Mbao? Kwa sababu mashabiki waliamini hakuwa na uwezo kama Kocha Msaidizi, Masoud Juma ambaye ameondolewa.

Kwanini baadhi ya wachezaji wamekuwa wakilaumiwa kwa nyakati tofauti kwamba wameridhika na mishahara mikubwa na ndio maana timu haichezi vema? Mbona hatujawahi kusikia Waganga wakilaumiwa na mashabiki?

Simba ionyeshe njia. Kuelekea katika mapinduzi ya kweli ambao inapitia kwa sasa ijaribu kuwa mfano kwa wengineo. Mechi ikikataa inakataa tu. Ni kama ilivyokuwa katika pambano dhidi ya watani wao Yanga. Haikuwa na mjadala kwamba Simba ilikuwa vizuri kuliko Yanga hata kama ingeruhusu bao la kufungwa kwa bahati mbaya. Mpira hauchezwi chumbani.

Kwa mchezaji mwenyewe kama Dilunga, asikubali kufanya alichofanya hata kama ni kwa gharama ya kufukuzwa timu. Ajiulize kama Mbwana Samatta au Simon Msuva wangekubali walichofanya.

Wasingekubali hata kwa dawa. Wote kama ilivyo kwa yeye wana hadhi ya kuwa wanasoka wa kulipwa.

Wanaamini katika wanachokifanya kisayansi kabisa.

Bila ya vipaji wasingefika walikofika. Na kama amekubali kuingizwa katika kundi la wachezaji mastaa kama hili la SImba kwa ajili ya kushinda mechi kwa uwezo wao, nadhani isingekuwa dhambi kama angekataa kushirikishwa alichofanya.