JB, Mboni wadai Mazembe wanakufa Taifa

Muktasari:

Upande wake Mboni alisema lazima hao TP Mazembe wakae huku akimuomba JB ampige picha akiwa nyuma ya Bus la Simba baada ya nyota wa timu hiyo kushuka.

 MSANII wa Bongo Movie, Jacob Steven 'JB' akiwa na mtangazaji wa kipindi cha The Mboni Talk Show maarufu kwa Jina la Mboni Masimba ametamba kuwa dawa ya TP Mazembe wataitoa muda mchache ujao.

JB ambaye amekuwa mbele kwenye michezo mbalimbali ya Simba kwa hata kwenda kambini kwao muda mwingine, alisema uwanja wa taifa sio sehemu salama kwa timu yoyote. Msanii huyo, alisema kinachompa jeuri ya kusema hilo ni kutokana na ubora wa kikosi chao na rekodi walionayo kwenye uwanja huo.

"Hii ni Simba lazima watu watambue, tumekamilika kwenye kila idara, najivunia kikosi chetu chenye wachezaji ambao wanaweza kuamua matokeo ya ushindi muda wowote. "Hapa Mazembe wanakufa tatu, nimeona vile wachezaji walivyokuwa na morali ya juu, " alisema JB akiwa na Mboni ambao kwa pamoja walikuwa wakikishudia kikosi cha Simba kikishuka kwenye Bus lao.

Upande wake Mboni alisema lazima hao TP Mazembe wakae huku akimuomba JB ampige picha akiwa nyuma ya Bus la Simba baada ya nyota wa timu hiyo kushuka. Zoezi hilo lilipomalizika JB na Mboni walielekea ndani ya uwanja wa taifa katika eneo lao la VIP kwa ajili ya kusubiri mtanange huo kuanza.