Ishu ya Redondo ilikuwa nzito

KWA mashabiki wa Simba wanamfahamu zaidi kwa jina moja la Redondo. Aliwahi kuwapigia kazi nzuri sana kabla ya kutua Biashara United ya Mara. Anaitwa Ramadhan Chombo Redondo. Siku hizi ana rasta, zamani alikuwa na mzuzu na dredi.

Redondo alipachikwa jina hilo la utani akifananishwa na kiungo wa zamani wa kimataifa wa Argentina, Fernando Carlos Redondo.

Ni mmoja wa viungo bora wenye udambwi dambwi uwanjani kuwahi kutokea nchini ambaye mpaka sasa bado anacheza soka huku akisema kuwa ana miaka mingine mitano mbele ndipo afikirie kutundika daruga.

Redondo anasema maisha ndani ya Biashara United ni mazuri na anafurahia. “Katika timu ndogo zinazojitahidi kuhudumia wachezaji wake vizuri hii ni mojawapo kwani hakuna stress, tunalipwa kwa wakati,tunatimiziwa mahitaji yote hivyo kazi yetu ni kucheza mpira.

“Msimu huu tuna malengo makubwa ya kufanya vizuri ikiwemo kumaliza ligi katika nne bora na naamini kama wachezaji wote tukitambua wajibu wetu na kupambana hakuna kinachoshindikana,” anasema Redondo.

Anaongeza: “Msimu uliopita tulifanya vizuri na wengi wakaannza kuifuatilia timu yetu na yote inatokana na juhudi za wachezaji lakini kubwa ni uwezo wa kocha wetu Francis Baraza ambaye amekuwa akituongoza kama baba, kaka na rafiki pia.

“Katika makocha ambao niliwahi kupita mikononi mwao, basi Baraza ni mmoja wa makocha bora sana ni kama alivyokuwa Patrick Phiri kipindi kile nacheza Simba. Ni mpole, mcheshi lakini mkali pale mnapoenda tofauti na kile anachotaka.Ukimuangalia anavyofundisha unaona kabisa huyu sio mwalimu tu ila ni mzazi pia lakini sifa yake kubwa ni ile hali ya kuwaamini vijana katika kikosi chake,” anasema Redondo.

“Kuna baadhi ya wachezaji nilicheza nao zamani akiwemo Mussa Hassan Mgosi, Athuman Iddi Chuji na wengine wengi wameshaaamua kustaafu lakini mimi bado bado kidogo kama miaka mitano mbele.

“Niko na kiwango kile kile mpaka sasa kwa sababu najua majukumu yangu na najitambua.Najitunza ikiwemo kufanya mazoezi kwa bidii, kupunguza vitu visivyo na msingi kwa mchezaji kwa sababu nataka siku nikiamua kustaafu basi nistaafu na utamu wangu,” anasema Redondo.

AKIRI SIMBA HAISHIKIKI

Redondo anasema licha ya kwamba Ligi Kuu Bara msimu huu imeanza na moto lakini Wekundu wa msimbazi wana balaa na timu nyingi zikijichanganya zitapigwa mabao mengi msimu huu.

Amekiri kuwa hata kipigo cha mabao 4-0 walichokipata kutoka kwa Simba Septemba 20 kilikuwa sio cha bahati baya kwami walizidiwa kila idara.

“Ligi msimu huu imeanza kwa ugumu sana na hali hiyo inatoa picha kuwa kazi itakuwepo kwani timu nyingi zimesajili wachezaji vijana ambao wanatoa ushindani mkubwa.

“Mpaka sasa timu ambayo naiona iko vizuri ni Simba kwani si umeona tulipigwa nne na niseme tu wale jamaa wakikuotea wanaweza kukupiga nyingi zaidi kwani kila mchezaji ndani ya ile timu ana uwezo wa kufunga,”anasema na kuchomekea kuwa kwenye timu za Tanzania bado kuna tatizo la uongozi.

“Ujue soka letu linashindwa kusonga mbele kwa sababu ya mifumo mibovu ya uongozi hasa kwenye hizi klabu kongwe Simba na Yanga yaani kila mtu ni kocha. Halafu zenyewe ndio zinazoongoza kufukuza makocha bila sababu za msingi.

“Tatizo la viongozi wa klabu hapa nchini kila mmoja anataka kuonekana kwamba yupo juu ya mwingine, hivyo wanashindwa kusimama katika nafasi zao vizuri, mfano kocha anapaswa kuachiwa majukumu yake kwa sababu ndio anawajua vizuri wachezaji lakini baadhi ya viongozi wanamuingilia na kubeba majukumu yasiyowahusu.

“Tanzania kila mtu kocha, mfano unakuta meneja anataka kupanga timu,kiongozi naye anapanga kikosi chake, mashabiki nao wana timu yao basi vurugu tu, hilo linamfanya kocha ashindwe kufanya kazi yake vizuri hasa kwa timu hizi kongwe.Halafu timu ikifanya vibaya kidogo tu anafukuzwa,” anasema Redondo ambaye ni mchezaji wa zamani wa Mbeya City na Ashanti United.

YONDANI NA YANGA

Katika kucheza kote soka kwenye Ligi Kuu Bara, Redondo anasema hakuna beki kama Yondani na ameshangazwa Yanga kuachana nae kienyeji.

“Sijajua hasa sababu iliyofanya Yondani akaondoka Yanga ingawa naamini bado alikuwa anastahili kuendelea kucheza ndani ya kikosi hicho kwa sababu ni beki mzuri na mzoefu.

“Ila kwa jinsi walivyomuacha naona sio sahihi. Hawajamtendea haki, walitakiwa kumpa heshima yake ili kama wanaachana waachane nae kwa amani kwa sababu Yondani ameitumia hiyo timu muda mrefu tena kwa kiwango bora

“Lakini unashangaa kwa sasa baadhi ya mashabiki wanamtukana Yondani na kumuona hafai kwa madai alikuwa anawahujumu.Hiyo inaonyesha jinsi mpira wa Bongo ulivyo mizengwe ,yaani mchezaji amecheza miaka tisa tena kwa kiwango kile kile , leo ndio useme anaihujumu timu? wakati wote walikuwa wapi,” alihoji Redondo.

WAZAWA WAAMINIWE

Timu nyingi hasa kubwa zimesajili wachezaji wengi kutoka nje hasa wa nafasi ya ushambuliaji jambo linalotishia nafasi ya wachezaji wazawa kucheza mara kwa mara katika vikosi hivyo.

Jambo hilo ni kama linamuumiza Redondo ambaye anasema ni jambo zuri kwa wageni kuwepo kwani wanaongeza ushindani lakini pia hata wazawa nao wapewe nafasi na waaminiwe katika timu zao.

“Huwa kuna msemo kuwa nabii hakubaliki kwao ndicho huwa kinatokea hata kwenye timu zetu kwani unaweza ukakuta wameletwa wachezaji wengi kutoka nje lakini wanataka wacheze wote na wazawa wanabaki benchi.

“Sio kwamba wazawa hawana uwezo hapana lakini kwa sababu tu kuna wageni lazima wacheze, lakini kama wazawa nao wakiaminiwa naamini watafanya vizuri kwani wanapocheza wageni tu itaiathiri hata timu ya Taifa na mwisho wa siku mzigo wote anabebeshwa Mbwana Samatta mpaka sasa tutamchosha”, anasema Redondo.

ISHU YAKE YA KUZAMIA

Usishangae, Redondo ameshawahi kujilipua na kuzamia nchini Norway lakini wakati akijiandaa kubadilisha uraia mambo yakabumbuluka na kurejeshwa nchini.

“Nakumbuka ilikuwa mwaka 2000 wakati huo niko katika kituo kimoja cha soka kinaitwa Youth Olympic Centre maskani yake ilikuwa Chang’ombe Dar es Salaam sasa tukaenda kushiriki mashindano vijana yaliyojulikana kama Gothia nchini Sweden na tukatwaa ubingwa baada ya kuwafunga Russia katika fainali.

“Mwaka 2002 tukaenda katika mashindano mengine kama hayo nchini humo sasa tukawa tunashauriana, mimi, Jabir Aziz na wenzetu wengine wawili kuwa kwa nini tusizamie huko huko maana timu nyingi zilikuwa zinatuhitaji baada ya kuvutiwa na uwezo wetu, hivyo tutapiga pesa.

“Tukamwambia kocha wetu alikuwa anaitwa Aluko Ramadhan kuwa kuna timu zinatuhitaji tunataka tubaki kucheza akaweka ngumu sasa wakati timu inajiandaa kurudi tukawatoroka na kubaki huko huko Sweden,bahati tulipata mtanzania akatusaidia kupata usafiri hadi Norway.Tulifika usiku sana na hatuna hata hela,” anasema Redondo

Anaongeza”Wakati tuko huko tulikuwa na bangili na cheni zile za utamaduni tukawauzia wazungu kwani walizipenda sana ndipo tukapata hela kidogo ya kula lakini hali ilipozidi kuwa mbaya ikabidi twende uhamiaji tukajilipua tukasema sisi ni wakimbizi kutoka Burundi tukabadili na majina na kwa sababu tulikuwa bado wadogo wakatukubalia hivyo tukawa tunacheza timu za huko.

“Wazungu walitupenda wakatupeleka hadi shule lakini tulipojaribi kuomba uraia wa kule ikawa ngumu kwani walisema Tanzania hairuhusu raia wake kuomba uraia wa nchi nyingine.Sasa mwaka 2004 ile timu yetu ya vijana ikaja Norway na wakaja na picha zetu wakitutafuta, baadae wakaondoka lakini wakati huo wenyeji wakatukamata kutupeleka uhamiaji wakatuhoji lakini tunawashukuru wale wenyeji wetu katika timu ya ligi daraja la pili ya Lyngdal walitutetea sana kwa sababu walitupenda hivyo tukaruhusiwa kubaki Norway.

“Tukakaa kama miaka mitatu, na mwaka 2007 kesi ikaibuka tena kuwa lazima turudi nyumbani kwa sababu tuliwadanganya kuwa ni wakimbizi kumbe sivyo, wakatuambia kwa sababu ni wadogo wanatusamehe ila lazima turejeshwe Tanzania na ingekuwa ni wakuwa wangetufunga jela. Basi ndio tukarejea nyumbani kwa usimamizi wao,” anasema Redondo.

Redondo ambaye alizaliwa Desemba 9, 1987, alianza kucheza soka la ushindani katika timu ya Friends Rangers kisha 2008 akahamia Ashanti United alipocheza nusu msimu kisha Simba kumsajili mwaka 2009.

Juni 2010 akasajiliwa na Azam aliyoichezea hadi mwaka 2012 na kisha kurejea Simba alipocheza hadi mwaka 2015 na kutimkia Mbeya City.