VIDEO: Ishu ya Fraga iko hivi

KIUNGO Mbrazil, Gerson Fraga alicheza dakika nane tu juzi na kuumia huku akitolewa akiwa amebebwa katika machela na watu wa huduma ya kwanza kwenye ushindi wa Simba wa mabao 4-0 dhidi ya Biashara United.

Baada ya kutolewa Fraga ambaye alianza katika mchezo huo, nafasi yake aliingia Said Ndemla aliyecheza mpaka mwisho.

Daktari wa Simba, Yassin Gembe aliliambia Mwanaspoti kuwa, mchezaji huyo aliumia goti baada ya kugongwa na mchezaji wa Biashara United maumivu ambayo yalimfanya kushindwa kuendelea.

Gembe alisema walimpa huduma ya kwanza Fraga pale uwanjani na jana walimpeleka hospitali ili kufahamu ukubwa wa tatizo.

“Tutamfanyia vipimo vikubwa zaidi hospitali ili kufahamu Fraga atakuwa amepata tatizo gani na matibabu yake yanatakiwa kwenda kwa namna gani,” alisema.

“Ni ngumu kueleza kama anaweza kuwa nje kwa muda gani kutokana na kuwa bado vipimo vya goti ambavyo tumekwenda kumfanyia havijatoa majibu yake na sasa anaendelea na matibabu ya kawaida.

“Matibabu ambayo tutampatia nina imani mambo yatakuwa mazuri na atarudi katika hali yake ya kawaida kama ilivyokuwa hapo awali, lakini kama kuna jambo lingine tutaeleza.” Tangu msimu huu uanze, Biashara United ndiyo ilikuwa mechi ya kwanza kwa Fraga kucheza katika kikosi hicho.