Ile tuzo ya mkali wa kuasisti England vita ni kali

Muktasari:

  • Msimu huu hawa hapa wanaoshindania tuzo ya kupiga asisti nyingi kwenye Ligi Kuu England. Nani atabeba?

LONDON ,ENGLAND . KWENYE Ligi Kuu England vita ni nyingi. Kuna wanaoshindania kubeba ubingwa. Kuna wanaochuana kuwania wabaki kwenye ligi wasishuke. Kuna vita ya kuwania ufungaji bora. Kuna vita ya kupambana kukamatia nafasi za nne za juu na vita nyingine ni ya kuwania kuwa mkali wa tuzo ya mchezeshaji bora wa msimu.

Mambo ni mengi, muda ni mchache. Kiatu cha Dhahabu vita yake ni kali na huko utakutana na wakali kama Mohamed Salah, Pierre-Emerick Aubameyang, Sergio Aguero, Harry Kane na wengineo. Shughuli unaambiwa hivi, ipo huko kwenye mchakamchaka wa kuwania tuzo ya mchezeshaji bora wa msimu, kwa maana ya staa anayeongoza kwa kupiga asisti kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Supastaa wa zamani wa Arsenal, Thierry Henry aliwahi kusema kwamba asisti ndicho kitu kilichokuwa kikimpa furaha zaidi kuliko kufunga mabao. Staa huyo hadi anaondoka kwenye Ligi Kuu England alipiga asisti 74 na anashika namba 11 kwa wakali wa muda wote waliopiga asisti nyingi kwenye ligi hiyo ya kibabe. Msimu huu hawa hapa wanaoshindania tuzo ya kupiga asisti nyingi kwenye Ligi Kuu England. Nani atabeba?

Mohamed Salah –Liverpool, asisti 7

Liverpool kwa sasa mekabana koo na Manchester City kwenye Ligi Kuu England, lakini yote hayo wana kila sababu ya kushukuru huduma ya supastaa wao, Mohamed Salah. Staa huyo amehusika kwenye mabao 24, akifunga 17 na kuasisti mengine saba. Kwa kitendo hicho, Mo Salah na asisti zake saba, anaingia kwenye vita ya kuwania tuzo ya mchezeshaji bora wa msimu huko kwenye Ligi Kuu England.

Joao Moutinho –Wolves, asisti 7

Kiungo fundi wa mpira kutoka Ureno, Joao Moutinho ametinga kwenye Ligi Kuu England na kuwashika. Anatoa huduma yake huko kwenye kikosi cha Wolves na kuingia kwenye orodha ya wakali wanaowania tuzo ya wakali wa asisti kwenye ligi hiyo msimu huu. Moutinho amepiga asisti saba, sawa na alizopiga Mo Salah na kufanya vita hiyo kuwa na utamu wa aina yake.

Paul Pogba –Man United, asisti 8

Tangu Ole Gunnar Solskjaer alipotua Manchester United, kiungo Paul Pogba anacheza soka la ubora wake kabisa. Kiungo huyo Mfaransa amekuwa akifunga na kuasisti mabao muhimu na kumfanya kwa sasa awe amefikisha asisti nane kwenye Ligi Kuu England na kumfanya aingie kwenye vita ya kuwania tuzo yam kali wa kuasisti kwenye ligi hiyo.

Pogba kwa kasi yake ya sasa ndiyo inayotishia zaidi na kuaminika kwamba huenda akawa tishio na kunyakua mzigo.

Raheem Sterling – Man City, asisti 9

Staa wa Manchester City, Raheem Sterling amekuwa kwenye kiwango bora kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Ametupia mabao 12 kwenye ligi hiyo katika mechi alizocheza na kuingia kwenye ule mchakamchaka wa kuwakimbiza kila Mo Salah kwenye vita ya Kiatu cha Dhahabu. Lakini, Sterling yupo kwenye vita nyingine ya kufukuzia tuzo ya mkali wa asisti kwenye Ligi Kuu England msimu huu akiwa amehusika kwenye kupiga pasi tisa zilizoleta mabao ya moja kwa moja kwa timu yake ya Man City yenye maskani yake huko Etihad.

Ryan Fraser –Bournemouth, asisti 9

Kiungo wa AFC Bournemouth, Ryan Fraser yupo bize pia kwenye kuwania tuzo hiyo ya wakali wa asisti kwenye Ligi Kuu England msimu huu kutokana na kile anachokifanya kwenye kikosi hicho. Callum Wilson anatisha kwa kufunga huko kwenye kikosi cha Bournemouth, lakini jambo hilo lisingekuwa rahisi kama kusingekuwapo na huduma ya mpiga pasi matata za mabao, Fraser, ambaye hadi sasa ameshapiga asisti tisa na kuwamo kwenye vita ya kuwania tuzo ya wapigaji mahiri wa asisti kwenye ligi hiyo msimu huu.

Christian Eriksen –Tottenham, asisti 9

Huko kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur, wachezaji kama Son Heung-min, Dele Alli na Harry Kane wamekuwa na sifa kubwa kutokana na uwezo wao wa kutupia nyavuni. Lakini, kwenye kikosi hicho kinachonolewa na Muargentina, Mauricio Pochettino kuna fundi wa mpira anayewezesha mabao hayo kupatikana na huyo si Christian Eriksen.

Kwenye Ligi Kuu England wakitajwa wapishi moto kwa msimu huu huwezi kuliweka kando jina la Eriksen, ambaye hadi sasa ameshapiga asisti tisa na ndio maana sio ajabu jina lake kuhusishwa na vigogo kama Real Madrid.

Leroy Sane –Man City, asisti 9

Kazi ya kufunga mabao huko Manchester City kwenye Ligi Kuu England inafanywa na straika wa Kiargentina, Sergio Aguero. Lakini, kasi ya kupiga asisti kwa msimu huu kwenye ligi hiyo, inafanywa vyema kabisa na staa wa Kijerumani, Leroy Sane.

Winga huyo matata kabisa kwa msimu huu amehusika kwenye asisti tisa na kuifanya Mann City kushika usukani wa ligi na kuweka hai matumaini yao ya kutetea ubingwa huo huku Liverpool wakiwaweka kwenye wakati mgumu kwa kulingana nao pointi, huku wenzao wakiwa bado na mchezo mmoja mkononi.

Hazard –Chelsea, asisti 10

Kwenye kikosi cha Chelsea mambo yangekuwa mabaya zaidi kama kusingekuwapo huduma ya staa wao, Eden Hazard kwa msimu huu. Chelsea kwa sasa inashika nafasi ya sita katika msimamo, lakini Hazard ndiye aliyehusika kwenye mabao mengi, 22, amefunga 12 na kuasisti mengine 10.

Kwa asisti zake hizo zilizofika tarakimu mbili, Hazard ndiye anayeongoza kwenye kinyang’anyiro hicho cha kuwania tuzo ya mkali wa kuasisti na kama ataendelea kwa kasi hiyo ya kuwapikia wenzake na wakafunga, basi anaweza kuibuka kibingwa msimu wa msimu.