Ikangaa, Bayi watoa kauli kujiuzulu Gidabuday

Tuesday November 5 2019

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Wakati Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) ukitarajiwa kuamua hatima ya nafasi ya katibu mkuu, Filbert Bayi na Juma Ikangaa wametoa maoni tofauti kuhusu sifa za mtendaji mpya ajaye.

Wakizungumza Dar es Salaam jana, wanariadha hao nguli wa zamani wametaja sifa anazotakiwa kuwa nazo mrithi wa aliyekuwa katibu mkuu wa shirikisho hilo Wilhelm Gidabuday.

Mkutano Mkuu wa RT utakaofanyika Desemba mkoani Dodoma, utatoa uamuzi wa katibu mkuu wa kujaza nafasi ya Gidabuday aliyejiuzulu wadhifa huo juzi.

Bayi bingwa wa zamani wa dunia alisema mrithi wa Gidabuday anapaswa kuwa na sifa ya kuongoza na anayefuata katiba ya chama.

“Awe muadilifu, mtu anayekubali kuulizwa, anawasiliana, mtu anayebeba tatizo la chama, aonyeshe ushirikiano na viongozi wenzake na akubali kujifunza,” alisema Bayi.

Ikangaa alisema katibu mpya anapaswa kuwajibika kwa kufuata miiko huku akishauri mtendaji huyo anapaswa kuajiriwa.

Advertisement

“Watakapokuwa na katibu wa kuajiriwa maadili yatakuwepo na hata uwajibikaji utakuwa wa kiwango cha juu kwa kuwa ni ajira yake na ataifanya kwa kufuata miiko, lakini kama si mwajiriwa hakutakuwa na masharti ya kumbana,”alisema Ikangaa.

“Hata TOC (Kamati ya Olimpiki Tanzania) ndiko tunaelekea tulikuwa tunasubiri maelekeo ya IOC (kamati ya kimataifa), kama riadha wataweza ni jambo jema sana,” alisema Bayi akiunga mkono kauli ya Ikangaa kuhusu katibu wa kuajiriwa.

Mwanariadha wa mbio fupi na Mtanganyika wa kwanza kushiriki Olimpiki ya mwaka 1964, Daniel Thomas alisema sifa ya mtendaji ajaye awe na uwezo wa kutafuta suluhisho la matatizo ya riadha.

Mwanariadha bingwa wa zamani wa dunia wa nusu marathoni, Fabiano Joseph alisema mrithi wa Gidabuday anatakiwa kuwa muadilifu katika utendaji wake.

Simbu afunguka

Nyota wa riadha Alphonce Simbu alisema amepokea kwa mshtuko taarifa za kujiuzulu Gidabuday kwa kuwa hakutarajia licha ya kufahamu RT kulikuwa na mgogoro.

“Alikuwa kiongozi ambaye alipenda mafanikio, sijui sababu iliyofanya ajiuzulu nitamfuta nizungumze naye,” alisema Simbu.

“Nitamkumbuka Gidabuday sijapenda kuondoka kwake najisikia vibaya lakini ndiyo imeshatokea,” alisema Fabiano.

Mwanariadha wa mbio ndefu za uwanjani Gabriel Geay alisema Gidabuday alikuwa tegemeo ndani ya taasisi hiyo, hivyo kuondoka kwake ni pigo.

Kauli ya Gidabuday

Wakati wadau hao wakitoa maoni, Gidabuday alisema ataendelea kushiriki riadha na anakwenda kuwa kocha wa kituo cha Hanan’g Sport cha kuibua vipaji vya mchezo huo.

“Sitaki kuzungumzia kilichosababisha nijiuzulu, lakini nitabaki kuwa mdau na kwenye mashindano ya Taifa mwakani naandaa timu yangu ambayo naamini itakuwa ya ushindani,” alisema Gidabuday jana.

Advertisement