Ihefu wao ni kukimbiza tu

KOCHA wa Ihefu FC, Maka Mwalwisi amesema ameishapata picha kamili ya namna Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), ilivyo msimu huu, hivyo ameamua kuja na mfumo wa kushambulia zaidi utakaopunguza kasi ya wapinzani wao.

Mwalwisi alisema baada ya kucheza na mabingwa watetezi Simba ambayo ina nyota wa kigeni na wazawa kuna kitu alikosoma ni namna gani akikutana na ushindani wa aina ile acheze ili kupata matokeo.

Vivyo hivyo alieleza uhalisia wa timu ambazo zinawachezaji wazawa kama Ruvu Shooting ambayo waliipiga bao 1-0, kujua jinsi yakucheza nazo, jambo analoona linampa mafanikio ya kile anachokitaka.

“Baada ya kucheza na Simba nimegundua nikikutana na timu za aina hiyo mfano Yanga na Azam FC, lazima nicheze kwa mbinu zaidi ili kuhakikisha tunapata matokeo, ndicho ninachowafundisha mazoezini na wachezaji wananielewa,”alisema na kuongeza kuwa.

“Mfano mifumo yangu ni kushambulia, hii ina maana kwamba ninakuwa napunguza kasi ya wapinzani kufika mara kwa mara kwenye lango letu kwani muda mwingi wao ndio wanakuwa wanatuzuia sisi,”alisema.

ACHAMBUA NYOTA WA KIGENI SIMBA

Anasema wakati wamecheza nao mechi ya ufunguzi ambayo walipoteza kwa mabao 2-1, aliona uwezo wa mastaa kama Clatous Chama, Joash Onyango na Meddie Kagere kwamba licha ya kucheza dakika chache lakini alikuwa mwiba kwa mabeki wake.

“Sio kila mchezaji wa kigeni ana kila kitu mbele ya wazawa, wengine wana uwezo upo sawa na wachezaji wetu, Chama, Kagere na Onyango wana kitu cha tofauti ambacho kinaleta uchangamfu kwenye ligi kwa hiyo nimiongoni mwa wale ambao wana kitu chakujifunza,”alisema.