Huyu kocha Aussems kumbe ni jeuri bwana

Tuesday February 19 2019

 

By Bertha Ismail

ARUSHA . KUKOSEKANA kwa washambuliaji wawili wa Simba, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere inaweza kuwa habari mbaya kwa mashabiki wa Simba ingawa kocha wao Patrick Aussems amewatoa hofu kwa kutamka kuwa hata bila nyota hao watapata ushindi dhidi ya African Lyon.

Simba leo Jumanne inatarajia kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Lyon kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa huku ikitoka kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga.

Okwi na Kagere wote wana kadi tatu za njano ambazo kikanuni hawaruhusiwi kucheza mechi hiyo, kadi hizo walizipata mechi dhidi ya Singida United, Mwadui FC ya Shinyanga na Yanga.

Mchezaji mwingine atakayekosekana kwenye mechi hiyo ni Mganda, Juuko Murshid ambaye alipata majeraha kwenye mechi yao na Yanga.

Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems amesema kukosekana kwa nyota hao hakuna maana kwamba watashindwa kupata ushindi kwani ana wachezaji zaidi ya 20 wenye uwezo wa kucheza soka la ushindani.

“Wachezaji hao wataukosa mchezo huu lakini mazoezini lazima waje kwa ajili ya kuwaandaa kuelekea michezo mingine inayokuja ikiwemo dhidi ya Azam pia safari ya kusaka nafasi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema.

Aussems alisema wachezaji wengi ambao hawajatumika katika mchezo uliopita ndio atawapanga leo hivyo wadau wa Simba wajitokeze kwa wingi kuona uwezo wa wachezaji wao sambamba na kusapoti timu yao ambayo kwa kipindi kirefu hawajaiona hasa wachezaji nyota wanaong’ara katika michezo mbalimbali.

“Arusha tumeona mashabiki wa kweli wamekuja kuipokea timu yao na hii inaonyesha walikuwa na kiu kubwa ya kuwaona nyota wao hivyo waje kwa wingi kuwapa sapoti na morali ya kufanya vizuri kwani pointi tatu ni muhimu kwetu kuweza kukaa nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wa ligi,” alisema Aussems

Lyon waidharau Simba

Wakati Simba ikitamba kupata ushindi bila nyota wao watatu, African Lyon nao wamewabeza wapinzani wao kwamba pointi tatu zitabaki kwao ili wajinasue mkiani.

Lyon ndiyo timu inayoshika mkia ikiwa na pointi 21 baada ya kucheza mechi 26 wakati Simba wao wamecheza mechi 17 wamekusanya pointi 39 wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo.

Kocha wa African Lyon Sulemani Jabir amesema “Tunawaheshimu Simba ni timu kubwa na ni maarufu, wana historia kubwa katika soka lakini tunaamini tutawapiga kwani wataingia uwanjani wakitudharau na wakijiamini.

“Simba kumfunga Al Ahly ya Misri na Yanga watatuona sisi cha mtoto, hiyo itatupa fursa ya kupata matokeo ndani ya dakika 90.

“Presha tuliyonayo si matokeo dhidi ya Simba bali matokeo na timu yoyote tutakayokutana nayo lengo ni kuondoka mkiani na kubaki ligi kuu ili mwakani tujipange zaidi,” alisema Jabir

Nahodha wa timu ya African Lyon, Jabir Azizi ‘Stima’ alisema; “Changamoto kubwa ni ratiba kubanana, ila tutapambana.”

Advertisement