Huyu akitua tu Yanga, mmekwisha

Thursday October 29 2020
yanga pic

STAA wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba amemwambia kocha mpya wa Yanga, Cedric Kaze kwamba kwa namna yoyote ile lazima atafute straika kwenye dirisha dogo la Desemba.

Mziba ambaye alitisha miaka hiyo kwa kufunga hasa mabao ya vichwa, alisema kila kitu kinaonekana kuwa sawa kwa Kaze, lakini lazima usajili wa dirisha dogo arudi sokoni kusaka mfungaji halisi wa mabao vinginevyo atajichelewesha kuchukua ubingwa. Dirisha dogo la usajili linafunguliwa Desemba 15 mpaka Januari 15.

“Kocha ameanza vizuri, sina wasiwasi na falsafa zake naona zitaifaa klabu, kwa jinsi alivyoanza binafsi nimefarijika na mwanzo wake lakini eneo ambalo lazima aliangalie kwa kina haraka ni straika mmaliziaji,” alisema Mziba.

Alisema Kaze anatakiwa kupata mshambuliaji halisi atakayetumia nafasi wanazotengeneza ili timu iweze kuwa na upana wa ushindi wake.

“Hawa washambuliaji alionao sasa sioni kama ufanisi wake utaweza kuja kwa haraka, lakini jinsi wanavyojipanga wananipa wasiwasi zaidi wanacheza mbali sana na lango la wapinzani,” alisema.

“Anatakiwa kupata mshambuliaji ambaye atakuwa hakai mbali na eneo la kufunga, nafikiri huyo ndiye mchezaji muhimu ambaye Kaze anatakiwa kuwa naye ili kikosi chake kitanue wigo wa kufunga zaidi.

Advertisement

“Ukiangalia Sarpong (Michael) na huyu Yacouba (Sogne) nilikuwa na imani nao sana, lakini naona nidhamu yao ya kutulia katika nafasi nzuri kutumia nafasi kwa sasa inaondoka taratibu.

“Sijui yule mshambuliaji mpya Ntibazonkiza (Said) kama atakuwa na ubora huo, kama ataweza kutulia eneo hilo basi anaweza kuja kuwa mfungaji bora na kuisaidia timu kuweza kuwa na ushindi mzuri,” alisema Mziba ambaye aliondolewa kwenye benchi la Yanga kama meneja hivi karibuni.

Alisema kikosi hicho sio kwamba hakitengenezi nafasi za kutosha, lakini shida ipo katika washambuliaji wa timu hiyo kujua kujipanga vyema ambapo kama atashindwa kuwapika inavyotakiwa lazima arudi sokoni kutafuta mfungaji halisi.

Aliongeza kuwa kwa morali iliyopo ndani ya kikosi cha Yanga kama watapata mshambuliaji huyo kisha akiangalia ushindani wa ligi kuna uwezekano mkubwa kikosi cha Kaze kikajiweka katika mazingira mazuri ya kuchukua mataji msimu huu.

“Ukiangalia Yanga na Azam ndizo timu ambazo zinajionyesha kuwa na mkakati mkubwa wa kuchukua mataji wakianzia mipango hiyo tangu wakati wa usajili wao, lakini pia wameanza vizuri, najua kwamba ligi bado lakini anayejipanga vyema mapema anaweza kuwa na hesabu nzuri.” Yanga itacheza na Biashara Jumamosi mjini Musoma.

 

Advertisement