Huyu Chama huyu!

Muktasari:

Simba ilipita robo fainali kwa kuing'oa Nkana FC kwa jumla ya mabao 4-3. Bao lililowavusha Simba lilifungwa na Chama dakika ya 89, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salam waliposhinda mabao 3-1.

Dar es Salaam. Achana na mambo yote yaliyofanywa na kiungo Mambia Cletous Chama ndani ya kikosi cha Simba lakini kutokana na mabao yake mawili aliyopiga kwenye mechi dhidi ya Nkana FC pamoja na AS Vita rekodi yake haitasahaulika.
Mabao hayo ndiyo yaliipeleka Simba hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo wao walipangwa Kundi D, pamoja na robo fainali inayotarajiwa kuchezwa Aprili mwanzoni.
Simba ilipita robo fainali kwa kuing'oa Nkana FC kwa jumla ya mabao 4-3. Bao lililowavusha Simba lilifungwa na Chama dakika ya 89, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salam waliposhinda mabao 3-1.
Chama alifunga bao hilo akipokea pasi ya Hassan Dilunga wakati la kwanza lilipachikwa na Jonas Mkude huku Meddie Kagere akipiga la pili.
Bao lingine la Chama lililowavusha Simba hatua ya robo fainali, lilifungwa dakika 89, mpira ukitoka kwa Haruna Niyonzima 'Fabregas'.
Hii ni rekodi ya pekee kwa Chama ndani ya Simba katika michuano hiyo mikubwa ya Kimataifa.
Hata hivyo, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems ametoa la moyoni baada ya Simba kuandika rekodi hiyo: "Ndani ya Simba,  Tanzania na Afrika Mashariki hili ni jambo kubwa. Simba ya sasa inazungumzwa kuhusu soka kwa Afrika Mashariki, asante kwa Simba."