Huyo Aiyee amepania kumfunika Makambo

Muktasari:

Aiyee alisema kiu yake ni kuongoza katika ufungaji na ushirikiano anaoupata kutoka kwa wanzake unampa matumaini ya kutimiza malengo yake.

MWANZA .STRAIKA wa Mwadui FC, Salim Aiyee juzi alifikisha mabao 10 akiwa nyuma bao moja kwa mshambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo mwenye mabao 11 na mchezaji huyo ametamka kumpita Mkongo huyo katika mechi ya leo Alhamisi dhidi ya Coastal Union.

Mwadui imetoka kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, itawakaribisha wapinzani wao hao katika Uwanja wa Mwadui Complex, uliopo Shinyanga.

Makambo raia wa DR Congo ndiye anayeongoza kwa ufungaji akifuatiwa na Aiyee, Eliud Ambokile (Mbeya City) na Said Dilunga wa Ruvu Shooting wakiwa na mabao 10 kila mmoja.

Aiyee alisema kiu yake ni kuongoza katika ufungaji na ushirikiano anaoupata kutoka kwa wanzake unampa matumaini ya kutimiza malengo yake.

Alisema licha ya kuwania tuzo hiyo, malengo mengine ni kuisaidia timu kupata matokeo mazuri na kujinasua kutoka nafasi za mwisho katika msimamo wa ligi.

“Nitaendelea kupambana kwa sababu natamani kuongoza orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu, malengo yangu ni kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri ili kukwepa rungu la kushuka daraja,” alisema Aiyee.

Kocha wa kikosi hicho, Ally Bizimungu alisema baada ya ushindi huo sasa wanahitaji pointi tatu nyingine kutoka kwa Coastal Union ili kujiweka katika nafasi nzuri.

Alisema kikosi chake kipo fiti na hakuna mwenye tatizo lolote hivyo watapambana kupata matokeo mazuri dhidi ya timu hiyo ya Tanga.

“Timu ipo vizuri na vijana wana ari na morari, kikubwa ni kuhakikisha hatufanyi makosa kwani wapinzani wametoka kupata ushindi mechi ya mwisho ugenini kwahiyo tutakuwa nao makini,” alisema Bizimungu.