Huku ama kule, Pochettino njiani jijini Manchester

MANCHESTER,ENGLAND. MAMBO yameiva pale nchini England kwenye Jiji la Manchester, ambapo kila kona jina la kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur limekuwa linatajwa kuja kuziba pengo moja kati ya mapengo mawili ambayo huenda yakaachwa na makocha wa sasa wa klabu hizo Ole Gunnar Solskjaer na Pep Guardiola ambao wana hatihati ya kubaki mwisho wa msimu huu.

Man United ndio inaonekana kuwa inahitaji zaidi saini ya kocha huyo kwa kuwa kikosi chao hakina muendelezo mzuri tangu kuanza kwa msimu ambapo kwenye michezo mitatu amepoteza miwili huku ikiambulia ushindi kwenye mchezo mmoja tu dhidi ya Brighton kwa bao la penalti ya dakika ya mwisho.

Lakini majirani zao Manchester City nao wanaonekana kuwa na mpango wa kumchukua Poch kwa kuwa Guardiola haonekani kuwa na mpango wa kutaka kusaini mkataba wa kuendelea kubaki baada ya msimu huu ambapo mkataba wake utakuwa umemalizika.

Pochettino, 48, hajapata timu ya kuifundisha kwa mwaka mzima baada ya kuondoka kwenye viunga vya White Hart Lane mwezi Novemba mwaka jana na dirisha lililopita la majira ya kiangazi alisema kwamba anataka kurejea England kwa kuwa amekusanya nguvu za kutosha jambo ambalo klabu hizo kutoka Manchester zilikuwa zinasubiri kwa hamu kubwa.

Man City ya Guardiola inaonekana kuwa katika hali mbaya baada ya kupoteza alama tano kwenye michezo yao mitatu ya mwanzo wa msimu huu wa EPL.

Ripoti zinadai kwamba Guardiola anaweza kurudi tena Barca baada ya mkewe Cristina, kuonekana katika Jiji hilo.

City ilishinda 3-1 katika mchezo wa kwanza dhidi ya Wolves kabla ya kukumbana na kipigo cha aibu cha 5-2 kutoka kwa Leicester kabla ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Leeds.

Pochettino alianza kufundisha soka mwaka 2009 katika klabu ya Espanyol kabla ya kujiunga na Southampton mwaka 2013 na akakaa kwa msimu mmoja na baada ya hapo akatua Spurs ambapo alipata mafanikio makubwa ikiwa pamoja na kuiongoza kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo alipoteza mchezo wa fainali dhidi ya Liverpool. Lakini alitimuliwa mwaka 2019 ikiwa ni muda mfupi baada ya kupata mafanikio hayo makubwa tokea aanze kufundisha ukocha.

Poch alihusishwa na dili la kwenda kuifundisha Barcelona kabla ya kuajiriwa kwa Ronald Koeman, lakini ilishindikana na moja kati ya sababu zilizotajwa ilikuwa ni kauli yake aliyowahi kuitamka kwamba kamwe hawezi kuifundisha klabu hiyo kwa vile kwenye damu yake kuna klabu ya Espanyol, ambayo ni mahasimu wa jadi wa Barcelona.