Hongera sana Taifa Stars, sasa Kamati ihamie Serengeti Boys

Muktasari:

Tunaupongeza uamuzi wa kuunda kamati kwa kuona umuhimu wa kufanya hivyo, hamasa iliyojengwa haikuwa ndogo kwani hata wachezaji wenyewe walipandwa na morari kiasi cha kucheza kwa nguvu zote.

Kwa takribani wiki mbili sasa, kulikuwa hamasa, hekaheka na amsha amsha za kuhamasisha mchezo wa jana wa Taifa Stars dhidi ya Uganda kuwania kucheza fainali za Afrika kule Cairo, Misri baadaye Juni-Julai.

Bahati nzuri mambo yamekuwa. Tanzania sasa inacheza fainali za Afrika ikitamba kutoka mataifa ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Hiyo ni miaka 39, sasa inaanza moja na kikubwa kinachotakiwa ni maandalizi mapema kuelekea kwenye fainali za Misri.

Tunaipongeza Kamati ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kazi kubwa kuhakikisha ushindi unapatikana lakini zaidi ya yote umati ambao wachezaji wameutendea haki.

Kimsingi, kamati imefanya kazi yake japo katika kipindi kifupi ikianzia kwenye mchezo wa Lesotho japo Stars ililala bao 1-0 na mechi ya jana kushinda dhidi ya Uganda.

Tunaupongeza uamuzi wa kuunda kamati kwa kuona umuhimu wa kufanya hivyo, hamasa iliyojengwa haikuwa ndogo kwani hata wachezaji wenyewe walipandwa na morari kiasi cha kucheza kwa nguvu zote.

Kwa kuwa kamati imefanya kazi yake inavyopaswa, kwanza tunashauri, suala la kamati lisiwe kama ilivyokuwa awali, kwamba tumeibuka dakika za mwisho. Kazi hii ifanyike mara baada ya ratiba kutangazwa.

Mfano, ratiba ya Kombe la Dunia Kanda ya Afrika itakapotoka, palepale kazi inaanza. Tusisubiri dakika za mwisho ndipo tunaianza kazi.

Kombe la Dunia Kanda ya Afrika inakuwa katika makundi na mshindi wa kila kundi ndiye atakayefuzu. Hapa Tusifanye makosa, mlango wa Afcon funguo yake imepatikana sasa itafungua mlango wa Kombe la Dunia.

Fainali zijazo za Kombe la Dunia zitafanyika Qatar 2022 inawezekana kama tukijipanga na tukasema; Zamu yetu na sisi Qatar 2022.

Jambo la pili kubwa ambalo liko mbele yetu kwa sasa, kwa kuwa Kamati inapumzika kidogo masuala ya Taifa Stars, yale majukumu, malengo na maelekezo yote ya kamati sasa yahamie kwenye timu ya U-17 ya Serengeti Boys.

Tunafahamu kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa fainali za vijana chini ya miaka 17, zinazoanza siku 19 zijazo hapa jijini Dar es Salaam.

Serengeti Boys imepangwa Kundi A pamoja na Uganda, Nigeria na Angola.

Wenyeji wataanza kampeni kwa kucheza na Nigeria kwa mujibu wa ratiba, sasa ni wakati wa Kamati ya Taifa Stars kutengeneza mazingira kama ambayo yamefanyika kwa Taifa Stars na ssa iwe kwao Serengeti Boys.

Tunafahamu Serikali ya Awamu ya Tano inataka kuona Tanzania inang’ara katika kila eneo la michezo kimataifa zaidi.

Ndio maana Rais John Magufuli, wakati akiikabidhi Simba ubingwa wa Ligi Kuu aliwaambia wajipange kuiwakilisha Tanzania, na leo hii wamefika robo fainali Afrika.

Pia Rais alisema kuwa atakuwa tayari kusimamia eneo hilo kwa ajili ya mafanikio ya Watanzania kwa kuwa Watanzania wanapenda michezo.

Kuonyesha kuwa Watanzania wana ari, moyo na mapenzi ya dhati kwenye michezo na ndio maana walifurika Uwanja wa Taifa na hata wengine wakakosa nafasi.

Kimsingi, vijana wa Serengeti Boys pamoja na kazi na jukumu tulilowapa kutuwakilisha, Kamati itaongoza kutengeneza hamasa, motisha na hilo litasaidia kuwajenga kisaikolojia kwa mechi zao.

Hamasa inaondosha woga, hamasa inamfanya mchezaji kuamini ameshinda na kujitambua na ndicho kinachotakiwa kwa wachezaji na zaidi ndicho kilichowatia nguvu wachezaji wa Taifa Stars kushinda.

Katika siku 19 zijazo, tuwape hamasa Serengeti Boys na kutokana na hilo, watakuwa wakicheza huku moyoni wanajua kuwa kupandishiwa bendera na kupigiwa wimbo wa taifa ni heshima na ni deni kubwa mbele yao wanalotakiwa kulilipa. Deni litalipwa kwa ushindi. Hakuna namna nyingine.

Watanzania wanasubiri kuona Serengeti Boys inafanya kile wanachotaka na si kingine ni ushindi.

Kamati ifanye kazi yake baada ya kumaliza jukumu la kuivusha Taifa Stars kwenda Misri na zaidi kuisimamia Serengeti Boys.

Kinachotakiwa sasa ni kwa wachezaji kucheza kwa nguvu, ari na malengo na kuwa makini katika maeneo muhimu na zaidi watambue Watanzania wanataka ushindi.