Homa ya Lionel Messi yapanda Manchester United

Muktasari:

  • Messi hajafunga bao lolote katika hatua ya robo fainali kwa mechi 11 zilizopita. Bao lake la mwisho alifunga dhidi ya PSG mnamo mwaka 2013 na tangu hapo mechi za robo fainali hana bahati nazo ingawa amekuwa moto katika mechi nyingi.

MANCHESTER, ENGLAND.LEO Jumanne katika Ligi ya Mabingwa Ulaya pale England ni Liverpool na Porto pale Anfield, halafu Tottenham itacheza na Manchester City lakini homa ya Lionel Messi kutua na Barcelona na kucheza na Manchester United kesho Jumatano Old Trafford ni kubwa zaidi.

Messi, mmoja kati ya wachezaji bora kuwahi kutokea duniani alitazamiwa kutua jijini Manchester leo na kisha kufanya mazoezi na wenzake jioni katika Uwanja wa Old Trafford kabla ya kuikabili United kesho na tayari ameanza kuzua gumzo.

Staa huyo wa kimataifa wa Argentina aliyetwaa ubingwa wa Ulaya mara nne na Barcelona anatua Manchester akiwa na rekodi mbili za kutatanisha. Moja inawapa matumaini, rekodi nyingine inawanyima nguvu Manchester United.

Messi hajafunga bao lolote katika hatua ya robo fainali kwa mechi 11 zilizopita. Bao lake la mwisho alifunga dhidi ya PSG mnamo mwaka 2013 na tangu hapo mechi za robo fainali hana bahati nazo ingawa amekuwa moto katika mechi nyingi.

Inaweza kuwa rekodi nzuri kwa Manchester United, lakini rekodi ambayo itakuwa tishio kwa United ni ile ya Messi kufunga mabao 22 katika mechi 30 alizocheza dhidi ya timu za Kiingereza.

Messi ndiye mchezaji aliyezifunga zaidi timu za Kiingereza katika michuano hiyo kuliko mchezaji yeyote.

Staa wa zamani wa Manchester United, Dwight Yorke ambaye aliisaidia United kutwaa mataji matatu kwa mpigo mwaka 1999 ikiwemo la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuichapa Bayern Munich mabao 2-1 Nou Camp ametoa neno kuhusu Messi.

Yorke anaamini hakuna namna ambavyo Manchester United inaweza kumzuia Messi asiwe na madhara kwa mechi zote mbili kuanzia Old Trafford kisha Nou Camp, isipokuwa wanahitajika kucheza kikamilifu kujaribu kutinga nusu fainali.

“Sidhani kama tutaweza kumzuia Messi. Inabidi uwe makini na mchezo wako tu. Nadhani inabidi tuicheze mechi kwa ukamilifu mkubwa kama tunahitaji kushinda. Tunajua Messi hapana shaka ni mchezaji bora zaidi duniani katika kizazi hiki na ukiwa akili umeweka kwake tu basi mambo yatakuwa magumu.”

“Lakini kama tukicheza kitimu, pamoja na ubora wa Messi nadhani tutakuwa na nafasi dhidi yao. Hata hivyo, unahitaji bahati katika hizo mechi mbili. Kama tukiipata bahati hiyo usiku wa kesho, hakuna sababu kwa nini Manchester United isondoke na ushindi wa jumla katika mechi mbili,” aliongeza Yorke.

Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer ambaye alikuwa na Yorke katika kikosi kilichotwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 1999 pale Nou Camp huku akifunga bao la pili katika pambano dhidi ya Bayern Munich, Jumamosi alikuwa uwanjani kumtazama Messi na wenzake katika pambano la Ligi Kuu ya Hispania dhidi ya Atletico.

Katika pambano hilo lililochezwa Nou Camp, Solskjaer alikumbushwa na Messi kuhusu ubora wake baada ya kufunga bao la pili katika pambano hilo huku bao la kwanza likifungwa na Luis Suarez ambaye naye anatazamiwa kuwepo katika pambano la kesho.

United itaingia uwanjani ikiwa na nguvu baada ya kupenya kwa maajabu katika hatua ya mtoano kwa kuichapa PSG mabao 3-1 jijini Paris licha ya kuchapwa mabao 2-0 katika uwanja wao wa nyumbani Old Trafford.

Solskjaer anajua endapo atapoteza katika mechi ya kesho Old Trafford United itakuwa katika nafasi ngumu ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya kusuasua katika ligi.