Hizi hapa Mashine za kazi Fenerbahce

TANGU kuondoka kwa Raul Meireles, Dirk Kuyt, Moussa Sow na Emmanuel Emenike kwenye kikosi cha Fenerbahce, miamba hiyo ya soka la Uturuki imekuwa ikiambulia patupu mbele ya Besiktas na Galatasaray.

Ni misimu mitano sasa imepita, ubingwa wa Ligi Kuu Uturuki ‘Super Ligi’ kwa Fenerbahce imekuwa hadithi tu ambayo wamekuwa wakiisikia kwa wapinzani wao Galatasaray ambao ndani ya miaka hiyo wamechukua mara tatu huku Besiktas wakibeba mara mbili.

Wakati ambao walikuwa wakikiwasha kina Kuyt ambaye aliwahi kuwika akiwa na Liverpool, Meireles aliyeichezea Chelsea kilikuwa kipindi cha neema kwa mashabiki wa timu hiyo na msimu wao wa mwisho kupata raha mashabiki hao ulikuwa 2013/14.

Miaka imekatika kutoka kizazi hicho hadi sasa ambapo kikosi cha Fenerbahce kina sura kadhaa mpya ikiwamo ya nahodha wa timu ya taifa la Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta ambaye amejiunga na timu hiyo akitokea Aston Villa ya Ligi Kuu England.

Samatta na wenzake wamebeba matumaini ya kurejesha zama za furaha kwa mashabiki wa Fenerbahce. Akiwemo nahodha huyo wa Taifa Stars hawa hapa ni nyota wengine ambao wanaweza kuipa ubingwa klabu hiyo kama ilivyokuwa zama za kina Meireles, Kuyt, Sow, Emenike na wengineo.

ALTAY BAYINDIR

Ni mdogo kiumri lakini mambo yake ni makubwa awapo golini. Ndiye kipa namba moja wa kikosi cha Fenerbahce alifanya kazi kubwa Altay Bayindir kwenye mchezo wake wa nne msimu huu dhidi ya Fatih Karagumruk.

Bayindir mwenye miaka 21, aliokoa mkwaju wa penalti wa Erik Sabo na kuisaidia Fenerbahce kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 huku wakiwa pungufu, Mauricio Lemos hakumaliza mchezo kutokana na kadi mbili za njano ambazo alionyeshwa.

GOKHAN GONUL

Licha ya kwanza kwa sasa Gokhan Gonul ndio anamalizia soka lake kutokana na umri kumtupa mkono anaonekana kuwa bado yumo na msimu huu tayari amefungua akaunti take ya mabao dhidi ya Caykur Rizespor pamoja na kuwa ni beki wa kulia.

Mbali na uwezo alionao wa kucheza beki ya kulia pia Gonul ni kiongozi mzuri awapo uwanjani ndio maana aliteuliwa kuwa nahodha wa timu hiyo.

JOSE SOSA

Kiungo wa zamani wa AC Milan, Jose Sosa amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu kwenye kikosi cha

Fenerbahce kabla ya mchezo wa jana dhidi ya Goztepe amefunga bao moja na kutoa asisti jingine.

Sosa ni mchezaji mzoefu ambaye amewahi kuichezea timu ya taifa lake la Argentina.

MBWANA

SAMATTA

Usajili wake ulikuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu, Fenerbahce walikuwa kwenye vita moja na Aston Villa kabla ya kuzidiwa kete na sasa ni furaha iliyoje kumpata mchezaji ambaye alikuwa kwenye rada zao baada ya mambo kumwendea vibaya nchini England.

Tayari mambo yameanza kumnyookea Samatta akiwa na Fenerbahce kutokana na kile ambacho alianza kukifanya kabla ya wiki ya kimataifa kwa kuiwezesha klabu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Fatih Karagumruk. Alifunga mabao yote mawili.

DEMBA CISSE

Huyu alikuwa pacha wa Demba Ba pale Newcastle United kwa sasa yupo zake Uturuki na Fenerbahce bado hajaanza kuonyesha mavitu kwenye Ligi lakini ni mshambuliaji wa daraja la juu ambaye anapewa nafasi ya kufanya makubwa akiwa na Samatta.

Wiki iliyopita kwenye wiki ya kimataifa Fenerbahce ilikuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Istanbulspor AS katika mchezo huo, Cisse alitupia moja wakati chama lake likiibuka na ushindi wa mabao 3-2.

ENNER VALENCIA

Kama ambavyo ilikuwa kwa Samatta na Cisse, Valencia naye alisajiliwa wakati wa dirisha lililopita la usajili akitokea Tigres UANL ya Mexico.

Ni mchezaji hatari ambaye amekuwa na uwezo wa kushambulia akitokea pembeni, aliwahi kucheza Ligi Kuu England akiwa na klabu mbali tofauti ambazo ni Everton na West Ham.

LUIZ GUSTAVO

Ndiye mchezaji mwenye jina kubwa zaidi kwenye kikosi cha Fenerbahce pia mwenye mafanikio zaidi, ikumbukwe kuwa kiungo huyo wa Kibrazil alikuwa sehemu ya kikosi cha Bayern Munich msimu wa 2012/13 kilichobeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ni kiungo mkabaji mwenye uwezo mzuri wa kutumia guu lake la kushoto kuchezesha timu, Bayern ilimnasa akitokea VfL Wolfsburg. Aliichezea miamba hiyo ya soka la Ujerumani na mwishowe kutimkia zake Ufaransa kabla ya kwenda Uturuki.

DIEGO PEROTTI

Mashine nyingine ya kazi ambayo ilikuwa ikifanya makubwa na AS Roma ya Italia, Diego Perotti ambaye pia aliwahi kuichezea Sevilla ya Hispania naye ni miongoni mwa wachezaji hatari kwenye kikosi cha Fenerbahce.

Muargentina huyo, anaweza kuwa sehemu na mafanikio kwa Fenerbahce kutokana na viashiria kadhaa ambavyo vimeanza kuonekana kikosini.