Hivi tunaitakia mema Simba kuipeleka Mapinduzi?

Muktasari:

Kocha Patrick Aussems ndoto zake kubwa ni kuiona Simba ambayo kwanza ameiwezesha kufuzu kwenye hatua ya makundi ya klabu bingwa Afrika lakini akitamani kuiona Klabu hiyo ikifika angalau hata robo fainali ili aweze kujitofautisha na baadhi ya makocha waliowahi Fanya hivyo kwa nchi hii kuanzia Yanga ya Makundi ya 1998 , Simba ya makundi mwaka 2003 hadi huku kwenye Kombe la Shirikisho barani Afrika hakuna Kocha aliyefika hatua hiyo yeye Aussems anatamani afanye hivyo.

Nilimsikia vizuri Kocha Mkuu wa Klabu ya Simba ambayo kwa sasa inakabiliwa na michuano mikubwa barani Afrika kwa ngazi za vilabu bwana Patrick Aussems akijaribu kujiingiza kwenye Uzalendo wetu kuhusu michuano ya Kombe la Mapinduzi ingawa unaona kabisa anaongea kwa Shingo Upande basi tu sababu nchi yenyewe anayoishi ndivyo hivyo.

 Kwa ufupi hajaridhika na namna Simba inajiandaa kuelekea mchezo wa Jumamosi ijayo unaowakutanisha wao Simba na JS Saoura kutoka Algeria, Aussems anasema kabisa kuwa hiyo njia ya kuiandaa timu huku mkishiriki michuano mingine siyo sahihi kabisa, tusiojua tunasema wachezaji wanatakiwa wacheze mechi hizo eti kuimarisha kikosi, sijui wachezaji wapate Utimamu wa mechi , pia sijui Mwalimu azidi kuwapa nafasi wachezaji asiowatumia ili wapate utimamu wa miili, yaani sisi tunajua kuzidi Aussems !!

 Aussems anajua kabisa kuwa kushiriki michuano hiyo ya Kombe la Mapinduzi huku ukiwa unajiandaa na mchezo mwingine wa kimataifa ni vitu viwili tofauti, hii ni Tukio la muda mfupi ambalo timu inaweza isitilie mkazo hili ni tofauti na kucheza ligi sababu kucheza ligi ni kusudio kubwa la kila timu duniani kuwa unashiriki ligi ili liweze kukupa ushindi wa uwakilishi wa nchi kimataifa, hili si tukio la muda mfupi ni tukio la muda mrefu lenye malengo makubwa, michuano aina hii kama Mapinduzi inafanana na ilitakiwa kuchezwa mapema kabla ya ligi kuu za Tanzania bara na Zanzibar kuanza hii ni michuano ya awali tu na ilitakiwa kubaki hivyo, bahati nzuri nchi hii tunaishi kijamaa na kufanya kazi zetu za mpira kikawaida sana.

Kocha Patrick Aussems anajua kabisa kuwa huwezi kuweka mkazo katika michuano miwili yenye malengo tofauti, leo unaiandaa timu kuelekea mchezo wa Klabu bingwa ya Afrika lakini kesho tu una mchezo  wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya Chipukizi ambayo kiuchezaji , kimbinu, kiuwezo na kila aina haifanani na uchezaji, mtazamo na mengineo kutoka JS Saoura, unawezaje kuweka mkakati mzuri wa kupambana na AS Vita huku  baada ya wiki kadhaa huku kesho yake unacheza dhidi ya Mlandege timu isiyo na mfanano wala lolote linalokaribia kuifikia AS Vita!

 Aussems alitamani kama ni michuano hii labda ingefanyika Dar kwenye kiwanja ambacho Simba watakitumia yaani Uwanja Mkuu wa Taifa , ili Simba iendelee kuuzoea na kuepuka majeraha mengi miongoni mwa wachezaji ambao kwa sasa wanatumia kiwanja cha Nyasi bandia ambacho kuumia ni rahisi  zaidi na hivyo kuatayarisha ushiriki wa wachezaji muhimu wa kikosi cha kwanza, Aussems anatamani michuano hii ingeshirikisha timu angalau waalikwa zenye uwezo mkubwa mfano wangeendelea kuja KCCA, Vipers za Uganda, Gor Mahia na kadhalika ambazo zingeweza kuipa Simba ushindani wa Nguvu, Aussems alitamani kuiona Simba ikicheza michezo pengine miwili tu ndani ya michuano hii ambayo ingeweza kumpa nafasi Kocha Patrick Aussems kurekebisha makosa ili baadaye timu iweze kufanya vizuri.

Bila shaka kwa Kocha Patrick Aussems ndoto zake kubwa ni kuiona Simba ambayo kwanza ameiwezesha kufuzu kwenye hatua ya makundi ya klabu bingwa Afrika lakini akitamani kuiona Klabu hiyo ikifika angalau hata robo fainali ili aweze kujitofautisha na baadhi ya makocha waliowahi Fanya hivyo kwa nchi hii kuanzia Yanga ya Makundi ya 1998 , Simba ya makundi mwaka 2003 hadi huku kwenye Kombe la Shirikisho barani Afrika hakuna Kocha aliyefika hatua hiyo yeye Aussems anatamani afanye hivyo.

Kila kitu kinawezekana iwapo tu Simba kama Klabu watamuangalia Patrick Aussems nini anakiwaza na kutaka kukifanya, licha ya matukio mengine yanayoihusisha timu yake kufanyika nje ya uwezo wake lakini ni vizuri kutumia mawazo yake ili atakaposhindwa basi Simba wote wawe wameshindwa na si Aussems peke yake.

Simba wanatakiwa kujua kuwa wachezaji wao huenda wakachoka haraka sana ndani ya muda mfupi hawa wachezaji walionao si vyuma na wala hakuna jicho la muono wa mbali kuwa Klabu yao ina kikosi Kipana , badala yake ni kuelewa kuwa kila Kocha huwa ana kikosi chake cha Ushindi na siyo kuwa na kikosi kipana hivyo si rahisi hata pale Kocha anapotaka kukibadili kikosi haiwezi kubadili wachezaji wa timu yote badala yake kuna kundi la wachezaji ambao ni lazima tutawaona wakizunguka tu kila timu inapocheza, hivyo Kwa Simba hii kuendelea kushiriki kila michuano yoyote inapoletwa badala yake tutarajie mshika mbili moja litamponyoka

Unaweza usiamini kama kweli Simba wanayaangalia yote haya na hujui Nguvu na mawazo yao wameyaelekeza wapi, kwa nini Shirikisho linashindwa kuisaidia Klabu hii hata kimawazo lakini zaidi haikuwa rafiki kuikubali michuano ya Sport Pesa kufanyika January huku ligi zote zikiwa zinaendelea ikimanisha timu za Simba, Yanga, Singida Utd na Mbao zitazidi kuongeza viporo vya mechi zao na kuifanya ligi kutoleta radha nzuri kama ilivyotakiwa.

Wakati Kocha na kikosi cha Simba kikiendelea kushiriki michuano hiyo huku mawazo ya Aussems yakiwa zaidi Dar es salaam kuelekea mchezo mkubwa wa kimataifa dhidi ya JS Saoura , wiki moja baadaye kikosi cha Simba kitalazimika kujitupa tena kuhakikisha wanashiriki michuano mingine ya Sport Pesa Cup michuano ambayo ina manufaa kibiashara zaidi kwani inamlipa mshindi wa kwanza zawadi kubwa ya fedha na kuipa Klabu bingwa ya michuano hiyo nafasi ya kucheza na timu ya ligi kuu nchini Uingereza Everton, hata hivyo michuano hii haikutakiwa kuchezwa katikati wakati ligi za nchi hizi za Kenya na Tanzania ikiendelea wakati Simba inajitayarisha na michezo mingine ya kimataifa mwishoni mwa wiki za kila mwezi , michuano hii ambayo huko awali angalau ilikuwa inafanyika wakati hasa ligi ya Tanzania ikiwa imemalizika na inaonekana kuwa inatumika kama michuano ya maandalizi ya timu kuelekea ligi zao.