Hivi Afrika Mashariki tulijiandaa kweli na Afcon?

Wednesday June 26 2019

 

By Boniface Ambani

FAINALI za Afcon 2019 zilianza rasmi nchini Misri Ijumaa kwa mchezo wa ufunguzi baada ya sherehe za kufana za michuano hiyo mikubwa Afrika inayofanyika nchini Misri.

Misri walifungua dimba dhidi ya Zimbabwe na kuwalaza bao 1-0 na kuvuna alama tatu baada ya Mahmoud Hassan Trezequet kupachika bao hilo la kwanza na la kipekee katika mechi hiyo. Kwenye michuano hiyo, zinashiriki nchi 24 zikiwemo za nne za Ukanda wa Afrika Mashariki, Uganda, Kenya, Tanzania na Burundi.

Katika ukanda wetu huu mambo si mazuri baada ya timu zetu tatu kuanza vibaya, Burundi ikianza kwa kichapo dhidi ya Nigeia cha bao 1-0, Kenya na Tanzania zikifuatia kwa kukubali vipigo vya mabao 2-0 kila moja.

Naipongeza Uganda ‘Cranes’ kwa ushindi wao wa mabao 2-0 dhidi ya DR Congo uliochezwa Jumamosi, mabao ya mshambuluaji Kaddu wa KCC Kampala na Emmanuel Okwi wa Simba ya Tanzania yakipeleka shangwe nchini Uganda.

Kikubwa nilichokiona na kukifurahia kwa Waganda ni ile hali yua kujiamini. Walipiga soka safi mno wakimiliki mpira, huku mabeki na washambuliaji walikuwa fiti kuanzia Godfrey Walusimbi, Khalid Aucho, Farouk Miya, kwa jumla walipiga soka safi.

Mchezo wa Nigeria dhidi ya Burundi ulikuwa wa kuvutia pia na Burundi walionyesha soka la zuri ingawa walizembea kidogo na kuruhusu bao lililowapa Nigeria alama tatu katika kipindi cha pili.

Advertisement

Jumapili usiku ndo haikuwa siku ya kutamani kabisa baada ya Tanzania na Kenya zote zikiwa Kundi C. Ni mechi ambazo zilitupa aibu kutokana na walivyocheza. Inawezekana vipi ndani ya dakika 90 Watanzania wanashindwa kupiga shuti hata moja? Nilishangaa mchezaji ambaye kocha anatarajia kumpigia mabao, John Bocco aligeuka mkabaji dakika zote.

Simon Msuvu na Mbwana Samata hawakuonekana kabisa. Kwa mtazamo wangu, Tanzania ni kama iliwazawadia Senegal mabao yale.

Niliuona ujasiri wa Aishi Manula ambaye aliokoa madhara mengi langoni mwake. Ilikuwa ni mechi ya Senegal dhidi ya Manula wakiibuka na ushindi huo wa mabao 2-0. Ni wazi ameshajiuza kutokana na kiwango alichoonyesha. Pongezi sana kwake.

Baada ya mchezo huo wa aibu wa Tanzania dhidi ya Senegal, baadaye ukafuata wa Kenya dhidi ya Algeria na mambo yakawa yale yale.

Hakuna hata shuti moja tu walilompigia kipa wa Algeria. Wachezaji wote kuanzia kwa mabeki, kiungo cha kati na washambuliaji ni kama hawakuwepo. Sikuiona Stars yenye ukomavu.

Walionekana ni kama imeokotwa tu maeneo ya Kariakor, jijini Nairobi na kwenda kushiriki. Kwa timu ambayo imekuwa ufaransa kwa zaidi ya wiki mbili kambini kucheza vile, ni Mungu tu. Hawakuwa na maelewano.

Itakuwa ni vigumu kushinda dhdi ya Senegal katika mchezo wao ujao kama hali itaendelea kuwa hivi. Mchecheto ulionekana kuanzia kwa mlinda lango Patrick Matasi ambaye alionekana kubabaika saana.

Kocha Sabastian Migne ana kazi kubwa ya kufanya kabla ya mechi zao za makundi kumalizika, bila hivyo, Stars itarejea Kenya baada ya mechi yao ya pili dhidi ya Senegal.

Kukosa wachezaji wenye uzoefu katika mechi za kimataifa katika ukanda huu, kwa kweli kumeonyesha kabisa ulegevu wetu. Washambuliaji wa Kenya walionekana butu sana. Viungo vilevile hawakufanya la maana.

Ni wazi ukanda huu una kazi kubwa ya kufanya. Ikumbukwe tukipoteza mechi ya pili ndio basi tena tunarejea Nairobi.

Tanzania na Kenya lazima tujikubali kwa mechi zinazofuata. Ni changamoto kwetu kuhakikisha tunashinda mechi zijazo kwa kuzifunga Algeria watakaocheza na Tanzania na Senegal watakaocheza na Kenya. Kila kitu kinawezekana. Ni kuamua tu kuheshimu na kulinda bendera za mataifa yetu kama wafanyavyo wanariadha kwenye mashindano makubwa.

Naamini kwenye soka tunaweza pia na hivyo tusiwaangushe Wanaafrika Mashariki.

Advertisement