MAONI YA MHARIRI: Hili halikwepeki, hatma ya soka letu lipo mikononi mwetu

Monday May 13 2019

 

SIKU zilizobaki kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 ambazo Tanzania kwa mara ya pili tutazishiriki zinahesabika.

Ni kama siku 41 tu kwa sasa ndizo zimesalia pia kwa timu ya taifa, Taifa Stars kutupa karata yake ya kwanza katika fainali hizo zitakazofanyika nchini Misri ikishirikisha timu za nchi 24 zilizofuzu mchujo kwa kuvaana na Senegal ya kina Sadio Mane. Tanzania inashiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza tangu waliposhiriki zile za mwaka 1980 zilizofanyikia Nigeria.

Bila shaka ni wakati wa kuionyesha Afrika hatukubahatisha kwenda Misri katika fainali hizo kwa kuhakikisha tunapata matokeo mazuri kwenye kundi C tulilopo sambamba na majirani zetu wa Kenya, Algeria na Senegal. Nafasi tuliyoipata tuitolea jasho kwani, licha ya Chama cha Soka Tanzania, FAT (sasa TFF) kupanga mikakati na kutaka kuona timu ya taifa, Taifa Stars ikikata tiketi ya ushiriki wa michuano hiyo, lakini bila mafanikio.

Kwa miaka 39 tuliisotea, nafasi hiyo na sasa tumeipata, hivyo ni wajibu wa kuandika rekodi hasa ikizangatiwa, kwa muda mrefu kumekuwa na mipango mkakati inayopangwa na klabu, TFF na hata serikali ili kuona Tanzania inaondokana na unyonge.

Unyonge katika michuano ya kimataifa, kwani kwa ngazi za klabu mafanikio pekee ya kujivunia ni Simba kufika fainali ya michuano ya Kombe la CAF mwaka 1993 na nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika) 1974.

Rekodi nyingine ni kufika robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika kulikofikiwa na Yanga mwaka 1969 na 1970 na Simba mwaka huu, pia kutinga kwa timu hizo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mwaka 1998, 2003 na 2019.

Pia Yanga na Malindi zimewahi kufika robo fainali ya michuano ya Kombe la Washindi kwa miaka miwili mfululizo, 1995 na 1996 na mwaka jana Yanga ilitinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ukiachana na rekodi hizo, uwakilishi wa klabu za Tanzania katika michuano ya kimataifa na hata ushiriki wa timu ya taifa za Tanzania kwenye anga hizo ni majanga, ukiondoa mwaka 2009 Tanzania ilipoenda fainali za Chan na safari hii tena katika Afcon 2019.

Ukiwasikia viongozi wa TFF ni kwamba wana kiu kubwa ya kutaka kuona klabu na timu za taifa za Tanzania zikifanya vema kwenye michuano ya kimataifa, hata ukisikiliza kauli za wanasiasa na viongozi wa klabu ni kuona timu zetu zikipeperusha vyema Bendera ya Taifa.

Lakini jambo la kujiuliza ni kweli tuna dhamira ya dhati ya kufanikisha jambo hilo kwa timu zetu za taifa na klabu kushiriki michuano ya kimataifa kama washindani na kupata mafanikio kama timu za mataifa mengine?

Kwa namna mambo yanayoendeshwa katika soka letu ni vigumu kufika huko kunakoliliwa na wadau wengi wa soka. Hatuwezi kupata wawakilishi bora wa nchi kama kuna hila, mipango na upendeleo katika soka letu. Hatuwezi kufika mbali kama hakuna mipango ya kuwaandaa wachezaji kucheza kwa kutegemea vipaji vyao na sio mipango ya nje ya uwanja kama ilivyopo katika soka letu. Soka letu linadidimizwa na mambo mengi, ikiwamo maamuzi ya utatanishi viwanjani yanayofanywa na waamuzi kwa maagizo ya viongozi wa soka ama kwa ushawishi wa milungula.

Klabu zinazotumia mamilioni ya fedha kusajili wachezaji na makocha wa kigeni na bado zinaendelea kutembeza fedha kuhonga waamuzi na wachezaji wa timu pinzani zitaweza vipi kufanya vema kwenye michuano ya kimataifa?

Ni vigumu hata kwa wachezaji wao kujiamini uwanjani kwa vile wanawaona na kusikia viongozi wao wanavyohaha kununua matokeo, huku TFF ikishindwa kusimamia kanuni, sheria na taratibu za soka kwa timu zote kwa sababu tu ya hisia za kishabiki walizonazo viongozi na wajumbe wa shirikisho hilo na kamati zake.

Kifupi ni kwamba hakuna njia ya mkato ya mafanikio mpaka pale wadau wa soka nchini watakapokaa chini na kuamua sasa ni lazima tubadili mfumo na uendeshaji wa soka letu kwa kuangalia wenzetu walipopita ndipo tutafanikiwa.

Ndio maana Mwanaspoti linaamini hatma ya soka letu lipo mikononi mwetu wenyewe na wala hakuna atakayekuja kutusaidia kwa sababu kupanga na kuchagua na kila mchuma janga daima hula na wakwao. Hivyo katika kuonyesha tunabadilika tuhakikishe Stars inaenda kufanya kweli Misri, kama ambavyo Simba ilivyojitutumua mbele ya vigogo katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kutoka robo fainali. Inawezekana!

Advertisement