Hiki Ndio Kinachowafelisha AZAM FC

Muktasari:

Walibeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2012-2013 na Kombe la Kagame mwaka 2015. Wameshiriki Kombe la Shirikisho lakini hawakuwa na mafanikio yanayoendana na uwekezaji wa pesa nyingi waliofanya.

KATIKA timu ambazo Afrika Mashariki inazitambua kwa uwekezaji wa maana ni matajiri wa Chamazi, Azam FC. Wana uwanja na miundombinu ya kisasa zaidi nchini jambo ambalo linaibua maswali juu ya kusuasua kwao kwenye michuano mbalimbali.

Walibeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2012-2013 na Kombe la Kagame mwaka 2015. Wameshiriki Kombe la Shirikisho lakini hawakuwa na mafanikio yanayoendana na uwekezaji wa pesa nyingi waliofanya.

Haina maajabu mbele ya Simba na Yanga. Hata hivyo, kuna mambo ambayo yanaonekana kuiharibia zaidi Azam kupata mafanikio ndani ya uwanja na kama wakituliza akili na kuweka mambo sawa mbona hawa Simba na Yanga watatulia na kuyasikia mataji kwenye luninga tu.

KUBADILISHWA KWA MAKOCHA

Hili ni tatizo kubwa ambalo limeonekana kuwa janga kubwa kwa Azam. Imekuwa kawaida kwa Simba na Yanga kubadili makocha karibu kila msimu, lakini sasa sumu imeanza kuingia huko Chamazi. Ajira za makocha wa Azam zimeanza kuwa njiapanda pale Chamazi kwani, imejikuta ikiingia kwenye mkumbo wa wababe hao wa soka la Bongo.

Tangu kupanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara mwaka 2007, Azam imepita kwenye mikono ya makocha zaidi ya 10 wa ndani nje ya nchi. Baadhi yao ni Mohamed King, Neider dos Santos, Itamar Amorin, Stewart Hall, Boris Bunjak, Joseph Omog, George Nsimbe, Zeben Hernandez, Aristica Cioaba ambaye amekifundisha kikosi hicho kwa mara ya pili wakati huo nafasi ya ukocha ikishikiliwa na Idd Cheche aliyekuwa anasaidiana na Meja Abdallah Mingange.

Kwa hesabu za haraka ni kwamba, mabosi wa Azam ni kama hawafahamu wanataka kitu gani. Staili ya kubadilisha makocha kila wakati imekuwa ikiwaadhiri sana katika kufikia mafanikio ndani ya uwanja.

Si kwamba, kasi yao katika kubadili makocha inafanana na ile ya Simba na Yanga, lakini kwa Azam ilistahili kukaa na kocha mweye ubora kwa muda mrefu ili kutengeneza misingi na kusuka kikosi cha muda mrefu. Tayari, wana timu za vijana zenye wachezaji wenye vipaji, lakini kwa kuwa timu ya wakubwa kumekuwa na ingia toka huenda ikaathiri hata maendeleo ya makindo waliopo kwa sasa.

Kwa sasa, iko chini ya Cioaba ambaye hakuna uhakika wa moja kwa moja kama anaweza kudumu klabuni hapo katika kipindi cha misimu miwili ijayo.

Hili ni eneo ambalo Azam wanakwama kwani, athari za kubadili makocha zimekuwa zikionekana moja kwa moja kwenye matokeo ya uwanjani.

KUKOSA KIKOSI ENDELEVU

Hakuna ubishi Azam ni timu yenye akademi bora kwa sasa nchini. Hilo ni jambo la kujisifia kwani hata wachezaji wengi wa timu za Ligi Kuu Bara ni matunda ya akademi ya Azam Fc.

Lakini, licha ya kuwa na akademi ya mfano, bado haina kikosi cha kwanza endelevu mpaka sasa. Ngumu kufahamu kikosi cha kwanza cha Azam.

Hata hivyo, kuna wachezaji wachache kama Agrey Morris, Salum Abubacary ‘Sure Boy’ ndio wachezaji ambao panga pangua unawakuta kwenye kikosi cha kwanza cha Azam.

Wengine wengi wamekuwa wakianza na wakati mwingine hukaa benchi hivyo, Azam imekuwa ikibadilika mara kwa mara kama timu inayojiandaa na msimu mpya hivyo, inajaribu wachezaji wake kusaka kikosi cha kwanza.

Katika kipindi cha miaka mfululizo Azam imekuwa bora katika eneo la ulinzi kutokana na uwepo wa Razack Abarola, Bruce Kangwa, Agrey Morris, Yakub Mohamed na Nico Wadada kucheza kwa muda mrefu hivyo, kubadilika kwa maeneo mengine imechangia kwa timu hiyo kufanya vibaya.

WAUZA SILAHA

Soka ni pesa na wazi kwamba Azam pesa wanayo, lakini walianza kujiweka nyuma walipofanya ubanaji wa matumizi misimu mitatu iliyopita.

Hilo lilisababisha kuwapoteza mastaa wengi ambao wamekwenda kuwa tishio ndani ya klabu zingine za Ligi Kuu Bara.

Baadhi ya nyota walioitosa Azam ni Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aishi Manula na John Bocco, ambaye kwa sasa ni nahodha wa Simba. Tangu wameondoka, Bocco na wenzake wamebeba mataji matatu ya Ligi Kuu Bara mfululizo huku Azam FC ikiendelea kuwa wasindikizaji licha ya kufanya usajili wa mastaa mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.

Usajili wa nyota wapya kama Never Tigere, Obrey Chirwa, Shaban Idi Chilunda, Iddi Nado na wengine bado haujairejesha Azam kwenye makali yake licha ya kutoa upinzani kwa vigogo hasa Yanga huku kwa Simba ikipigwa nje ndani.

LAZIMA WABADILIKE

Hivi karibuni Azam ilifanya mabadiliko kwa kugusa baadhi ya idara zake nyeti ili kwenda sambamba na ushindani. Bosi wa klabu hiyo Abdulkarim Amin ‘Popat’ anaonekana kuwa na mwanga wa kuifanya Azam kuwa bora zaidi.

Hata hivyo, ni lazima waende sambamba na mabadiliko na mahitaji ya kikosi chao. Kwa sasa Simba na Yanga zinapambana kwenye usajili kunasa mastaa wapya huku Azam ikiwa kimya. Ni lazima Azam FC ikunjue makucha yake kwa kuchuana jino kwa jino na Simba na Yanga ili isibaki kuwa wasindikizaji kwani, ni aibu kukosa michuano ya Caf wakati wana kila kitu.