Hii jezi mmh! Wachezaji watano, mabao 14 tu

Thursday June 13 2019

 

MANCHESTER, ENGLAND. UMESIKIA hii? Manchester United imeshindwa kumpata mrithi wa Cristiano Ronaldo hasa kwa kuangalia kile wachofanya mastaa walitua Old Trafford badala yake na kukabidhiwa jezi yenye namba aliyokuwa akivaa mahali hapo.

Ronaldo, alikuwa akivaa jezi namba 7 kwenye kikosi hicho cha Man United, ambapo aliondoka Juni 2009 na kwenda kujiunga na Real Madrid kwa ada iliyovunja rekodi ya dunia kwa wakati huo, Pauni 80 milioni.

Wakati Real Madrid wakipata mafanikio kwa kuwa na huduma ya Ronaldo kwenye kikosi chao, huko Man Unitd mambo yamekuwa majanga tu, hakuna aliyeza kuziba pengo lake. Tangu wakati huo Ronaldo alipoondoka, kuna wachezaji watano wamevaa jezi namba 7 ya Man United na walichofanya ni sifuri.

Ni hivi, wachezaji hao wote watano kwa ujumla wao, wamefunga mabao 14 tu kwenye Ligi Kuu England.

Wa kwanza kuvaa jezi hiyo alikuwa Michael Owen, ambaye licha ya kuwa moto anapokaribia goli, lakini alifunga mabao matano tu katika mechi 31 alizocheza kwenye ligi. Kisha alifuatia Antonio Valencia, ambaye hakuna alichofanya akiwa na jezi hiyo zaidi ya kuumia tu na kuamua kuitema.

Akaja, Angel Di Maria na kupewa jezi hiyo ambapo mashabiki wengi waliamini sasa Ronaldo amepata mrithi sahihi. Lakini, Muargentina huyo alidumu Old Trafford kwa msimu mmoja tu, akaondoka akiwa amefunga mabao matatu.

Advertisement

Ikafika zamu ya Mdachi, Memphis Depay akatua Old Trafford na kupewa jezi hiyo namba 7, ambapo alifunga mabao mawili tu katika mechi 16 alizoanza na 13 nyingine alitokea benchi. Naye akadumu kwa msimu mmoja na nusu akaondoka kwenye Lyon.

Kwa sasa jezi hiyo inavaliwa na Alexis Sanchez na kinachotokea ni majanga makubwa. Staa huyo kutoka Arsenal, ametua Man United akiwa analipwa pesa ndefu sana, lakini staa huyo amefunga mabao matatu tu katika mechi 32 alizocheza kwenye Ligi Kuu England huku kinachoripotiwa kwa sasa huenda akafunguliwa mlango wa kutokea huko Old Trafford na kocha Ole Gunnar Solskjaer.

Advertisement