Hii! kumbe Auba alikuwa wa Barcelona

Muktasari:

UMESIKIA hii? Kumbe Barcelona ilikuwa kwenye harakati za kutaka kumsainisha straika wa Arsenal na timu ya Taifa ya Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang lakini dili limekufa baada ya staa huyo kuongeza mkataba wa miaka mitatu ambao unamfanaya kuvuta Pauni 350,000 kwa wiki.

LONDON, ENGLAND

UMESIKIA hii? Kumbe Barcelona ilikuwa kwenye harakati za kutaka kumsainisha straika wa Arsenal na timu ya Taifa ya Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang lakini dili limekufa baada ya staa huyo kuongeza mkataba wa miaka mitatu ambao unamfanaya kuvuta Pauni 350,000 kwa wiki.

Tovuti ya Sky Sports inadai miamba hiyo ya LaLiga ilifeli kwenye aina ya dau aliloweka ili kumsainisha ambapo Arsenal iliona ni dogo na mwisho ikaamua kumuongeza mkataba.

Kocha mpya wa Barca, Ronald Koeman anahitaji kupunguza baadhi ya wachezaji na kusajili wachezaji wapya ambao anaamini watakuwa na ubora mkubwa kuliko waliopo kwenye timu kwa sasa. Na mchezaji ambaye ana asilimia kubwa za kuondoka ni Luis Suarez, hivyo itakuwa inahitaji kuziba pengo.

Klabu nyingine ilikuwa kwenye harakati hizo ni Inter Milan ambayo imeangukia pua baada ya Aubameyang kusaini mkataba mpya.

Aubameyang kwa sasa ni miongoni mwa wachezaji vipenzi wa timu hiyo.

Mkataba wa zamani wa mwamba huyo ulikuwa unamalizika Juni, 2021 hivyo ilikuwa inawafanya mashabiki wa Arsenal kuwa na hofu ya kumpoteza kwa kuwa mchakato wa kuongezea mkataba ulikuwa unachelewa.

Msimu uliopita alifunga mabao 22 na akamaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa wafungaji nyuma ya Jamie Vardyaliyefunga mabao 23. na msimu huu tayari ameanza kuonesha makali yake katika mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Fulham ambapo alifanikiwa kufunga wakati Arsenal ikishinda mabao 3-0.

Aubameyang amekuwa msaada mkubwa kwa Arsenal kutokana na kiwango chake kilichoisaidia kuipa ubingwa wa Kombe la FA na Ngao ya Jamii chini ya kocha Mikel Arteta.

Barcelona imekuwa kwenye hali mbaya baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye mbio za ubingwa mbele ya wapinzani wao Real Madrid sambamba na kupokea kichapo cha mabao 8-2 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa kutoka kwa Bayern Munich imewafanya kuanza kupambana kujenga safu yake ya shambuliaji.