Hebu msikie huyu kocha

KAMA kuna watu wana furaha na mzuka mwingi leo Jumatano basi ni mashabiki na mabosi wa Simba. Leo mashabiki watafurika pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwenye tukio kubwa na la kihistoria kusherekea Simba Day.

Lakini, ndani ya sherehe hizo kuna mambo mengi yametokea kwa wiki kadhaa sasa na leo wanahitimishwa rasmi.

Katika hitimisho hilo, Simba itatambulisha kikosi chake kipya kwa ajili ya kutetea ubingwa wake msimu huu, pamoja na benchi la ufundi ambalo linaongozwa na Mbelgiji, Patrick Aussems.

Mwanaspoti lililokuwa limeweka kambi sambamba na Simba kule Uturuki, linakupa kwa kifupi alichoahidi Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Ausemms na ipi mipango yake kwa timu hiyo.

Anasema, yupo ndani ya kikosi hicho kuhakikisha timu inaweka rekodi kitaifa na kimataifa, pia yuko tayari kwa Simba Day na mchezo wao dhidi ya Asante Kotoko anauchukulia kama sehemu ya maandalizi.

“Timu ipo vizuri lakini bado haijakaa sawa ninavyohitaji bado tuko katika maandalizi na hata mchezo wetu wa Simba Day ni sehemu ya maandalizi tu,” anasema Ausemms kocha aliyejiunga na Simba msimu huu baada ya kuacha kuinoa timu ya Taifa ya Nepal.

“Ninachowaambia mashabiki wa Simba, waje kwa wingi kuona timu yao inavyofanya, najua wana hamu kubwa ya kuiona. Kwa upande wa kiwango kwa sasa bado, kuwa na timu bora inahitaji muda wa kutosha.”

Kocha huyo, ambaye aliifundisha kwa mafanikio klabu ya AC Leopards ya Congo muda ndiyo filosofi yake anataka kuwa na kikosi kinachocheza soka na kupata matokeo uwanjani.

PATRICK NI NANI?

Patrick Winand Aussems alizaliwa, Februari 6, 1965 katika mji wa Moelingen, Ubelgiji na kuicheze RCS Vise kati ya 1974-81, klabu iliyokuja kufilisika mwaka 2014.

Patrick alikipiga pia Standard Liege (1981-88), kisha kutua K.A.A Gent (1988-19), R.F.C Seraing (1989-90) na ES Troyes AC (1990-93).

Baada ya kustaafu mwaka 1993 kama Kocha Mchezaji wa Troyes inayoshikili Ligue1, alijitosa jumla kuwa kocha ndani ya klabu hiyo hadi 1995 alipotua Saint Lousienne ya Re Union. Pia, amezifundisha Capricorne Saint-Pierre, Stade Beaucairois, Stade de Reims, KSA Cameroon, SCO Angers, Evian Thonon Gaillard F.C, Shenzhen Ruby, Chengdu Blades na kutua kwa waliokuwa Mabingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika 2012 AC Leopards akimpokea Joseph Omog aliyekuwa ameletwa nchini kuinoa Azam FC. Alianza kuinoa timu hiyo tangu mwaka 2013-15 ambapo chini yake aliisaidia Leopards kubeba taji la Ligi Kuu ya Congo msimu wa 2014.